• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
TAHARIRI: Wanasiasa watumie kampeni kuelewa matatizo ya raia

TAHARIRI: Wanasiasa watumie kampeni kuelewa matatizo ya raia

NA MHARIRI

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) hatimaye imeanza rasmi kuwaidhinisha wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali za kisiasa kwenye kinyang’anyiro cha Agosti 9.

Mnamo Jumapili, wanasiasa wanaotaka nyadhifa za kuanzia MCA hadi urais walianza kuwasilisha stakabadhi zao kwa maafisa wa IEBC kote nchini.

Pia hiyo ilikuwa siku ya kufunguliwa rasmi kwa msimu wa kampeni, zinazotarajiwa kuendelea hadi saa 48 kabla ya Uchaguzi, yaani Agosti 7.

Ingawa baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiendelea na kujipigia debe, wamekuwa wakifanya hivyo bila kufuata sheria. Kwa mujibu wa Katiba pamoja na Sheria ya Uchaguzi (2016), kampeni rasmi huanze kulingana na ratiba ya IEBC. Lakini baadhi ya wanasiasa walianza kampeni punde tu wapinzani wao walipoapishwa kuchukua nyadhifa bungeni.

Kwa muda huu wote ambapo wanasiasa wamekuwa wakiitisha mikutano ya kisiasa, ni dhahiri kuwa wamekuwa hawakosi umati wa watu. Hata ikiwa siku ya watu kuwa kazini, mikutano ya kampeni imekuwa ikijaa watu. Hili halitarajiwi kubadilika. Umati huo hata huenda ukaongezeka, huku watu wakijitokeza kusikiliza kama watapewa matumaini.

Kupatikana kwa umati ni ishara tosha kwa wanasiasa kwamba kuna upungufu wa ajira na shughuli za kuwapa mapato Wakenya. Mtu aliye na biashara yake, hawezi kuifunga eti kwa sababu mwanasiasa ametembelea mtaa wake akiwapa watu Sh500 wahudhurie mkutano. Watu walioajiriwa, hata siku kunapokuwa na Uchaguzi Mdogo, hubidi IEBC kuwaomba waajiri wawaachilie kwa dakika kadhaa wapige kura.

Ina maana kuwa, hakuna mwalimu anayeweza kuwaacha wanafunzi madarasani, mwendesha ndege anayeacha abiria, daktari anayeacha wagonjwa hospitalini akahudhurie mkutano wa kisiasa.

Kwenye mikutano hiyo, wanasiasa wamekuwa wakiwatajia vijana kuwa watapata ajira na kadhalika, kama maneno matamu tu ya kuwapumbaza.

Muda huu wa kampeni, yafaa utumike na wanasiasa kutazama na kujionea hali halisi ya wapigakura. Takwimu za majuzi zinaonyesha kuwa kiwango cha umasikini kimepanda nchini. Watu hawana pesa. Baadhi ya wanaohudhuria mikutano hiyo ya kisiasa hata hawajawapeleka shuleni watoto wao kujiunga na kidato cha kwanza.

Wengine huenda kwenye mikutano hiyo wakiwa na matumaini ya kupata angalau pesa za chakula cha watoto wao jioni hiyo. Hali ya maisha ni ngumu sana kwa wananchi.

Viongozi wanapoanza safari ya kutafuta kura, wanukuu masuala muhimu katika maeneo yao, ili wakiingia bungeni au katika afisi nyingine za uongozi, waunde sera za kuwasaidia wananchi.

Hakutakuwa na umuhimu kwa watu kupewa Sh500, mfuko wa unga au leso wakati huu, kisha wateseke kwa miaka mitano ijayo.

You can share this post!

Mchakato wa kuuzwa kwa Chelsea unakamilika rasmi leo Mei...

WANDERI KAMAU: Amerika ikome kufumbia macho uozo unaoikabili

T L