• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
WANDERI KAMAU: ‘Deni’ ametuacha nalo Kibaki kwa kutoandika wasifu wa maisha yake

WANDERI KAMAU: ‘Deni’ ametuacha nalo Kibaki kwa kutoandika wasifu wa maisha yake

NA WANDERI KAMAU

MOJA ya sababu kuu ambazo zimeyapa uhai matukio yaliyofanyika karne nyingi zilizopita duniani ni uandishi wa vitabu.

Pasingekuwapo na uandishi wa vitabu au majarida kueleza jinsi matukio hayo yalivyofanyika, pengine yangesahaulika kitambo sana.

Narejelea matukio muhimu kama vile uumba wa dunia, mchipuko wa falme kubwa na muhimu kama Roma, Ugiriki; vita vilivyozuka katika baadhi ya mataifa ya Ulaya kuziondoa tawala za kifalme, biashara ya utumwa iliyoendeshwa na baadhi ya Wazungu na Waarabu, kutokea kwa Vita Vikuu vya Kwanza na Pili vya Dunia (1914-1918 na 1939-1945), ukoloni barani Afrika kati ya matukio mengine.

Ni kupitia uandishi wa vitabu ambapo hadi leo, vizazi vya sasa bado vinasoma historia kuhusu watawala maarufu kama Julius Caesar (wa ufalme wa Roma), Alexander the Great, Mfalme Selemani, Adolf Hitler (licha ya ukatili wake) kati ya watawala wengine.

Pasingekuwapo na uandishi wa vitabu, kizazi cha sasa hakingejua lolote kuhusu historia ya Kenya—historia kuhusu Vita vya Mau Mau (1952-1956), harakati za Ukombozi wa Pili wa Kisiasa (1980-1992) au harakati za kupigania Katiba ya sasa.

Licha ya sifa nyingi alizomiminiwa baada ya kifo chake, hayati Mwai Kibaki alituacha kwa deni kubwa la kihistoria.

Ikilinganishwa na viongozi wengine, Mzee Kibaki alifariki bila kuandika kitabu chochote kinachorejelea safari yake ya kisiasa tangu alipoanza kuhudumu katika serikali ya Mzee Jomo Kenyatta katika miaka ya sitini, hadi alipostaafu kama rais wa tatu wa Kenya mnamo 2013.

Mzee Kibaki amefariki bila kutuambia, kwa mfano, jinsi uhusiano wake ulivyokuwa na Mzee Kenyatta, marehemu Daniel Moi na vigogo wengine wa kisiasa aliohudumu nao katika serikali zilizopita.

Mzee Kibaki hakueleza lolote kuhusu safari ya masomo yake—kutoka mvulana aliyechunga mifugo katika kijiji cha Gatuya-ini, Othaya, Kaunti ya Nyeri hadi kuwa Rais wa Tatu wa Kenya.

Ametuacha kwa deni kubwa la kihistoria.

Hajafuata mkondo ulioigwa na baadhi ya vigogo wa kisiasa kama vile kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, aliyekuwa gavana wa Benki Kuu ya Kenya Duncan Ndegwa, mwanasiasa Jeremiah Kiere-ini kati ya wengine ambao wameandika vitabu vingi kueleza safari zao za kisiasa.

Changamoto kuu kwa sasa ni kwa washirika wa karibu wa Mzee Kibaki kuhakikisha kuwa wamenakili historia yake, ili kukifaa kizazi cha sasa na vile vitakavyokuja baadaye.

Ni muhimu kwao kulipa ‘deni’ hilo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Aliyejaza nafasi ya Usain Bolt ajitosa Kip Keino Classic

Uhuru na Ruto walimana kuhusu shida za Wakenya

T L