• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
WANDERI KAMAU: Kupuuza Okwach ndani ya timbo ni kubagua maskini

WANDERI KAMAU: Kupuuza Okwach ndani ya timbo ni kubagua maskini

Na WANDERI KAMAU

JAMII imemsaliti Tom Okwach, mmoja wa wachimba dhahabu ambaye bado amekwama katika timbo la dhahabu la Abimbo, Kaunti ya Siaya.

Leo, ni siku ya 28 tangu timbo hilo kuporomoka mnamo Desemba 2.

Kuna wenzake kadhaa waliookolewa wakiwa hai, ingawa wawili miongoni mwao walifariki na kuzikwa.

Tom bado amekwama. Familia yake haijapoteza matumaini. Imeeleza itafanya kila iwezalo kuhakikisha imepata mpendwa wao—awe hai au la.

Cha kusikitisha katika taswira hii ni jinsi karibu kila mmoja ameitekeleza familia hiyo.

Wameachwa peke yao kupambana na dhoruba kali lililoishinda serikali za kitaifa na kaunti.

Katika siku za mwanzo, waokoaji kutoka serikali ya Kaunti ya Siaya walipiga kambi katika mgodi huo kila siku. Walipata usaidizi kutoka kwa serikali ya kitaifa, ndipo wakafanikiwa kuwaokoa wachimba dhahabu kadhaa.

Hata hivyo, baada yao kuchoka, waliiacha familia ya Tom kukabiliana na kibarua kilichowashinda wao wenyewe.

Tangu wakati huo—karibu wiki mbili sasa—familia ya Tom imekuwa ikilia. Imeililia serikali ya kaunti, imeililia serikali ya kitaifa, imewarai wahisani, jamaa na marafiki—lakini bado inahangaika. Inahangaika katika dunia isiyo huruma wala msaidizi yeyote.

Serikali ya Kaunti ya Siaya ililalamikia gharama ya mafuta ya mashine za kuchimba timbo hilo kama sababu kuu ya kujiondoa.

Bila shaka, visingizio kama hivyo ndivyo vimetolewa na idara nyingine ambazo zimekata tamaa na kujiondoa kwenye harakati hizo.

Maswali yanayoibuka ni: Ikiwa vikosi vya serikali vimejiondoa katika zoezi hilo baada ya kushindwa, ni familia maskini italihimili dhoruba hilo kali? Mbona familia ya Tom inabaguliwa kwa njia ya wazi bila yeyote kujitokeza kuitetea? Ni kosa la mtu kuzaliwa katika familia isiyo tajiri?

Bila shaka, huu ni ubaguzi wa wazi. Ni dhihirisho tosha kuwa watu maskini katika jamii ya sasa huwa hawajaliwi hata kidogo. Hawana nafasi yoyote ikilinganishwa na watu matajiri.

Ni wazi kwamba ikiwa mkasa huo ungeikumba familia tajiri, kwanza tungemwona Rais Uhuru Kenyatta akituma rambirambi kwa “jamaa na marafiki” wa waathiriwa.

Pili, tungewaona vigogo wa kisiasa kama Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, Musalia Mudavadi (ANC), Kalonzo Musyoka (Wiper), Gideon Moi (Kanu) kati ya wengine wakitoa jumbe kama hizo, wakieleza jinsi “waliofariki walichangia ustawi na maendeleo ya nchi.”

Tatu, tungemwona Rais akitangaza siku maalum “kumwomboleza au kuwaomboleza” waliofariki.

Nne, serikali ingebuni kamati maalum ya watu mashuhuri kusimamia mipango ya mazishi ya marehemu.

Tano, upeo wa “hekima” kwa waliofariki ni kuandaliwa mazishi ya kitaifa, huku bendera zikiwa zimepeperushwa nusu mlingoti.

Ni tukio kisa cha kutamausha kinachopaswa kuizindua jamii kwamba uhai hauna tabaka.

[email protected]

You can share this post!

Viongozi wafokea wabunge kwa kupigana bungeni

JUMA NAMLOLA: Kuna maisha baada ya sherehe za kukaribisha...

T L