• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
WANDERI KAMAU: Raia wapewe mafunzo ya kukabili mikasa tofauti

WANDERI KAMAU: Raia wapewe mafunzo ya kukabili mikasa tofauti

Na WANDERI KAMAU

TOFAUTI kubwa iliyopo baina ya nchi nyingi za Afrika na mataifa ya Ulaya, ni mikakati ambayo huwa nayo katika kujitayarisha kukabili na kudhibiti mikasa.

Barani Ulaya, nchi nyingi huwa zimeweka mikakati thabiti ambayo huzisaidia sana kukabiliana vilivyo na mikasa yoyote inayoibuka; kama vile milipuko ya volkeno, tetemeko za ardhi na mafuriko.Ingawa mikasa hiyo huyakumba mataifa hayo mara kwa mara, mikakati ambayo imeweka kudhibiti athari zake ni ya kuridhisha kwa kiwango kikubwa.

Kwa mfano, katika nchi kama Ufaransa, huwa kuna somo la lazima katika kiwango cha shule za msingi na upili kuhusu hatua ambazo wanafunzi wanapaswa kuchukua wakati mikasa kama mafuriko inatokea.Hilo ni ikizingatiwa nchi hiyo ni miongoni mwa mataifa ambayo hukumbwa na mikasa ya mafuriko mara kwa mara.

Nchini Japan (barani Asia), huwa kuna somo maalum kwa wanafunzi katika viwango vyote vya elimu—shule za msingi, upili na vyuo vikuu—kuhusu namna wanapaswa kujilinda dhidi ya athari za mikasa kama tetemeko za ardhi.

Hata hivyo, hali ni kinyume barani Afrika, ambapo mitaala ya elimu iliyopo huwa haitilii maanani juhudi za kuwapa wanafunzi mbinu za kujitayarisha kukabili mikasa mara inapotokea.Pengo hilo ndilo limechangia maafa mengi kushuhudiwa wakati mikasa kama mafuriko inapotokea katika mataifa mengi barani humu.

Kwa mfano, kwenye mkasa wa basi uliotokea katika Kaunti ya Kitui mapema wiki hii ambapo zaidi ya watu 30 walifariki, pengo hilo lilidhihirika.Juhudi za uokozi zilitatizika sana kutokana na ukosefu wa watu wenye ujuzi wa kuogelea au kuwaokoa watu wanaosombwa na mafuriko.

Ni wapigambizi wachache tu ambao walikuwepo. Kutia msumari kwenye kidonda, wengi wao hawakuwa na vifaa vya kisasa vya kuogelea au kuwasaidia waathiriwa wa mkasa huo.Kwenye mkasa uliotokea katika eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya wikendi iliyopita, ambapo timbo la mawe liliporomoka na kuwazika watu kadhaa, tatizo hilo lilijitokeza pia.

Pengine mikasa hiyo, kati ya mingine ingezuiwa, ikiwa Wakenya wengi wangekuwa na ujuzi wa msingi kuhusu mbinu za kujinusuru wanapojipata katika hali hiyo.Ikizingatiwa serikali imekuwa ikiendesha mabadiliko ya elimu nchini kupitia Mfumo wa Elimu ya Umilisi na Utendaji (CBC), ni muhimu ijumuishe Somo la Ushughulikiaji wa Mikasa.

Hili litawasaidia pakubwa kupiga jeki vikosi vya uokozi vinapofika katika maeneo ya mikasa kuwasaidia waathiriwa.Vile vile, itakuwa hatua nzuri, inayowiana na uhalisia uliopo katika maisha ya sasa, ambapo mikasa mingi imekuwa ikiripotiwa karibu kila sehemu.

Kenya itakuwa imepiga hatua kubwa kwa kuhakikisha imewapa raia wake ujuzi muhimu kujiokoa wenyewe wanapokumbwa na mikasa kwa kushusha utegemezi wao kwa idara za [email protected]

You can share this post!

Mvurya aeleza sababu za kuunga naibu wake

Azimio la Umoja kumeza Jubilee, ODM

T L