• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
Mvurya aeleza sababu za kuunga naibu wake

Mvurya aeleza sababu za kuunga naibu wake

GAVANA wa Kaunti ya Kwale, Bw Salim Mvurya, amesimama kidete kumuunga mkono naibu wake, Bi Fatuma Achani, kurithi ugavana mwaka ujao wakati ambapo magavana wengine wanasitasita kuwaunga mkono manaibu wao.

Katika ukanda wa Pwani, Bw Mvurya pamoja na mwenzake wa Kilifi, Bw Amason Kingi na Hassan Joho wa Mombasa watakamilisha vipindi vyao vya pili vya ugavana mwaka ujao.Manaibu wa magavana katika kaunti hizo tatu, wameeleza maazimio ya kutaka kurithi viti hivyo ila ni Bw Mvurya pekee ambaye ameunga mkono wazi azimio la naibu wake.

Bw Mvurya ambaye alishinda kiti hicho kupitia Jubilee mwaka wa 2017 anasisitiza kuwa, uamuzi wake kumpigia kampeni Bi Achani ni kutokana na kuwa kuna kazi ambazo serikali ya kaunti bado inastahili kukamilisha.Alisema anaamini hilo litawezekana tu ikiwa zitaachwa mikononi mwa mtu ambaye anaelewa mahali ambapo safari nzima ilianza.

“Ninakaribia kumaliza hatamu yangu, ninamwamini naibu wangu wa miaka 10 kuendeleza miradi yetu ya maendeleo. Hatujafika kule tulipopania lakini tumejaribu kuleta maendeleo,” alisema Bw Mvurya katika mahojiano Jumatano.

Kulingana naye, Bi Achani amekuwa mwaminifu kwake na amejifunza masuala ya uongozi bora kutoka kwake.Aliwakashifu wapinzani wake kwa kuendeleza siasa za ukabila na jinsia wanapofanya kampeni dhidi ya Bi Achani, akidai kuna baadhi yao wanaompinga kwa msingi wa kuwa yeye ni mwanamke.

Mnamo Oktoba, Bi Achani alipigwa jeki baada ya Naibu Rais William Ruto kumuunga mkono na kumpigia debe akiwataka wakazi wa Kwale kumpigia kura. Hivi majuzi, Bw Mvurya pia alijitokeza wazi kutangaza ataunga mkono azimio la Dkt Ruto kwa urais mwaka ujao.

Bi Achani alitarajiwa kumenyana na Bw Lung’anzi Mangale kutafuta kupeperusha bendera ya Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kwa kinyang’anyiro cha ugavana Kwale mwaka ujao.Hata hivyo, Bw Mangale ambaye ni mfanyakazi wa Mamlaka ya Bandari za Kenya (KPA) ameonekana kusitasita kujihusisha na UDA tangu Bi Achani alipotangaza nia ya kutumia tikiti ya chama hicho.

Bi Achani ni miongoni mwa wanawake takriban 23 nchini ambao wamepanga kuwania ugavana mwaka ujao.Bw Mvurya alieleza kuwa, hatua zilizopigwa kimaendeleo katika uongozi wake pamoja na Bi Achani zinafaa kuzingatiwa na wapigakura, huku akitaka wapinzani pia wadhihirishe uwezo wao kutekeleza kiwango hicho cha maendeleo.

“Bi Achani ndiye anayefaa kuendeleza ruwaza yetu ya maendeleo. Serikali yangu imefanya maendeleo mengi hasa katika sekta za elimu, afya, barabara na kilimo. Ninawarai ifikapo uchaguzi wa Mwaka 2022 mumuunge mkono naibu wangu,” akasema.

Katika Kaunti za Kilifi na Mombasa, Bw Kingi na Bw Joho wako katika njia panda na wamekataa kutangaza wazi mwanasiasa ambaye wangependa arithi nafasi zao watakapostaafu ugavana.Kwa Bw Kingi ambaye anavumisha chama kipya cha Pamoja African Alliance (PAA), orodha ya wandani wake wanaotaka kiti hicho ni ndefu, hali inayomwacha ajikune kichwa.

Miongoni mwao ni naibu wake, Bw Gideon Saburi, kakake mdogo, Bw Michael Kingi ambaye ni mbunge wa Magarini, Spika wa Bunge la Kilifi, Bw Jimmy Kahindi, na afisa mkuu wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani Bw Emmanuel Nzai.

Kiti hicho kinamezewa mate pia na Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro aliyeingia Chama cha ODM kutoka Jubilee hivi majuzi, Mbunge wa Malindi Bi Aisha Jumwa anayetarajiwa kuwania kupitia kwa UDA, na balozi wa Kenya nchini Tanzania, Bw Dan Kazungu.

Wakati mwingi Bw Kingi huepuka mijadala kuhusu urithi wa kiti hicho.Kwingineko Mombasa Bw Joho, husisitiza kuwa hataidhinisha mwanasiasa yeyote kurithi kiti chake, huku orodha ya wale wanaotaka kiti hicho ikisheheni wandani wake wa kisiasa na kibiashara.

Baadhi yao ni naibu wake, Dkt William Kingi, Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir, na mfanyibiashara Suleiman Shahbal.Watatu hao wote wanatafuta tikiti ya ODM lakini Bw Joho huwaambia wamenyane bila kumtafuta.

Wanasiasa wengine wanaotaka kurithi kiti cha Bw Joho ni Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo (Wiper), aliyekuwa seneta wa Mombasa Hassan Omar (UDA), mfanyibiashara Awiti Bolo (UDF), Mohammed Bahaidar (UDA) na Sanjeev Agwaral (UDA).

You can share this post!

Wapiganaji wapora chakula cha msaada

WANDERI KAMAU: Raia wapewe mafunzo ya kukabili mikasa...

T L