• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
WANDERI KAMAU: Ruto atahadhari asirudie ‘hila’ za watangulizi wake

WANDERI KAMAU: Ruto atahadhari asirudie ‘hila’ za watangulizi wake

NA WANDERI KAMAU

KWA kawaida, raia huwa na msisimko mkubwa kila serikali mpya inapotwaa uongozi wa nchi yao.

Hili hutokana na ahadi ambazo hutolewa na viongozi wanaochaguliwa kuhudumu katika nyadhifa tofauti.Hata hivyo, hali hubadilika kulingana na mkondo ambao utawala husika huchukua.

Katika historia ya Kenya, tawala kadhaa zilionyesha matumaini makubwa, ingawa baadaye zilibadilika na kuchukua mkondo wa kutamausha.

Moja ya utawala huo ni ule wa Mzee Jomo Kenyatta. Alipochukua uongozi mnamo 1963, Mzee aliahidi kuwa serikali yake ingemheshimu kila mmoja. Kutokana na masaibu mengi ambayo Wakenya walikuwa wamepitia chini ya utawala wa wakoloni, Mzee Kenyatta aliahidi serikali yake ingewafuta machozi Wakenya, hasa mashujaa waliojitolea kwenda misituni kuwakabili Waingereza kupitia vita vya Mau Mau.

Hata hivyo, Mzee alianza kubadilisha mwenendo wake kadri miaka ilivyosonga. Badala ya kuwaliwaza Wakenya, serikali yake ilianza kuwahangaisha na kuwatesa. Badala ya kuhakikisha waliopoteza mashamba yao wakati wa vita vya Mau Mau walirejeshewa mali yao, waligeuzwa kuwa maskwota. Badala ya Mzee kurudisha mkono kwa waliojitolea pakubwa ili kuhakikisha ameachiliwa kutoka gerezani na Wazungu, aliwageuka wote. Kati ya viongozi hao ni Jaramogi Oginga Odinga.

Mielekeo iyo hiyo ndiyo walifuata marais wastaafu Daniel Moi (marehemu) na Uhuru Kenyatta.

Moi, kwa upande wake, alianza operesheni kali dhidi ya watu aliohofia walikuwa sehemu ya wale walipanga njama za kumpindua mamlakani 1982.

Baadhi ya wale waliojipata pabaya ni marehemu Charles Njonjo, aliyehudumu kama Mwanasheria Mkuu kati ya 1963 na 1980.

Vivyo hivyo, aliposhinda urais kwa muhula wa pili mnamo 2017, Bw Kenyatta aliwageuka watu waliomsaidia kwenye kampeni, akiwemo Rais William Ruto, baada ya kuanzisha ushirikiano mpya wa kisiasa na kiongozi wa Azimio, Bw Raila Odinga.

Cha kushangaza ni kuwa, licha ya ahadi yake ya kuzingatia Katiba, imeibuka kuna uwezekano Rais Ruto ameanza kuwaiga watangulizi wake. Kinaya ni kuwa, ‘dhambi’ zake zinaonekana kuwa na uzito mkubwa, hata kuliko za marais wa awali. Hili ni baada ya mbunge wa Fafi, Salah Yakub, kufichua mpango wa kuhakikisha Rais Ruto ameitawala Kenya kwa miaka 20 kupitia mageuzi ya kikatiba.

Ingawa chama cha UDA kimekanusha kauli ya mbunge huyo, ukweli ni kuwa viongozi wakuu serikalini na chama chenyewe wamebaki kimya.

Kwa mfano, Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua bado wameendelea kunyamazia suala hilo.

Je, huenda huo ndio ukweli?

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Chama cha Biden chafanya vyema chaguzi za kati ya muhula

Kalonzo, Muthengi wataka wakazi walipwe fidia kupisha...

T L