• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
WANDERI KAMAU: Teknolojia ya uchaguzi IEBC ingefanywa na vijana nchini

WANDERI KAMAU: Teknolojia ya uchaguzi IEBC ingefanywa na vijana nchini

NA WANDERI KAMAU

TANGU Kenya kujinyakulia uhuru kutoka kwa Waingereza mnamo 1963, moja ya ahadi kuu ambazo viongozi wa kisiasa wamekuwa wakitoa kwa vijana nchini ni kuweka mikakati kuhakikisha kuwa wamekumbatia mbinu muhimu za kiteknolojia.

Kwa kauli yao, ni kupitia mbinu hizo pekee ambapo Kenya inaweza kupiga hatua muhimu za kiuchumi na kuyafikia mataifa yaliyostawi kiviwanda kama vile Amerika, Japan, Ujerumani, Uingereza kati ya mengine.

Hata hivyo, ahadi hizo zimebaki kuwa hadithi tamu za Alfu Lela Ulela, ambazo huwa hazitimizwi hata kidogo.

Hatua ya viongozi kutotekeleza ahadi hizo ndiyo imeifanya Kenya kuendelea kuwa “mtumwa wa kiteknolojia” wa mataifa hayo.

Mfano halisi ni hatua ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutegemea kampuni kutoka mataifa ya nje kuendesha masuala yake ya kiteknolojia.

Kwenye uchaguzi wa mwaka huu, IEBC iliipa kandarasi kampuni ya Smartmatic kutoka Amerika kuendeleza na kulainisha masuala na mitambo yake ya kiteknolojia.

Isitoshe, tume hiyo ilitoa kandarasi ya kuchapisha karatasi za uchaguzi kwa kampuni ya Inform Lykos kutoka Ugiriki.

Hii si mara ya kwanza.Mnamo 2017, tume hiyo ilitoa kandarasi ya uendeshaji mitambo ya kiteknolojia kwa kampuni ya OT Morpho kutoka Ufaransa.

Bila shaka, mwelekeo huo unaonyesha kuwa taasisi kuu nchini hazina imani na ujuzi wa kiteknolojia walio nao vijana wetu.

Ikumbukwe kuwa, Kenya ni miongoni mwa mataifa yaliyopiga hatua kubwa sana duniani kwenye ustawishaji na uboreshaji wa teknolojia.

Barani Afrika, Kenya inaorodheshwa kuwa miongoni mwa mataifa tano bora kwenye uendelezaji wa teknolojia. Baadhi ya mataifa hayo ni Nigeria, Misri na Afrika Kusini.

Maswali yanayoibuka ni: Mbona tawala zilizopo huwa zinawasaliti vijana kwa kutowapa kandarasi kuendeleza baadhi ya masuala muhimu ya kiteknolojia?

Ni lini tutakoma kuwa “watumwa” wa mataifa ya kigeni katika karibu kila nyanja? Mbona tunadunisha weledi wa vijana wetu?

Taswira chungu ya uhalisia huo wa kusikitisha ni matatizo yaliyoshuhudiwa Jumanne, ambapo Mitambo mingi ya Kuendesha Uchaguzi (KIEMS) ilikumbwa na msururu wa hitilafu.

Katika baadhi ya maeneo, mitambo hiyo ilikosa kabisa kufanya kazi hata baada ya tume kuleta mitambo mbadala. Hili ni kinyume na hakikisho zake mwanzoni.

Tuna vijana wenye uwezo mkubwa kusimamia masuala yote ya kiteknolojia nchini, bila mwingilio wa wageni.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Sheria yafaa ibadilishwe mshindi wa uchaguzi...

Wanavoliboli wa KU wajiandaa kushiriki voliboli ya Kombe la...

T L