• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
WANDERI KAMAU: Tufufue BBI na kukumbatia mazuri yaliyopendekezwa

WANDERI KAMAU: Tufufue BBI na kukumbatia mazuri yaliyopendekezwa

INGAWA Idara ya Mahakama ilifutilia mbali utekelezaji wa Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI), ukweli ni kuwa baadhi ya mapendekezo yaliyokuwepo katika mswada huo yangeifaa nchi pakubwa.

Baadhi ya mapendekezo makuu yaliyokuwepo katika mswada huo ni kubuniwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani nchini, nafasi za Uwaziri Mkuu na manaibu wake wawili.

Ingawa Rais William Ruto na washirika wake waliendesha kampeni kali kuupinga mswada huo kama njama ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kubuni nafasi za kisiasa kwa washirika wake baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, ukweli ni kuwa, BBI ingeifaa nchi pakubwa, bila kujali mrengo ambao ungeibuka mshindi kwenye uchaguzi huo.

Tangu aanze kufanya teuzi mbalimbali katika serikali yake, Rais Ruto “amefufua” baadhi ya mapendekezo ya BBI, hali inayoibua maswali kuhusu sababu yake kuupinga mpango huo.

Kwa mfano, Katiba ya sasa haina nafasi ya Kiongozi wa Mawaziri, bali nafasi zilizopo katika Afisi ya Rais ni zile za Rais, Naibu Rais, Mwanasheria Mkuu na Baraza la Mawaziri.

Hivyo, kwa kumteua aliyekuwa kiongozi wa ANC, Bw Musalia Mudavadi kama Kiongozi wa Mawaziri, Rais Ruto ‘alivunja’ Katiba na kuifufua upya BBI.

Pili, kwa kutoondoa nafasi za Mawaziri Wasaidizi (CASs), ambazo zilibuniwa na Bw Kenyatta, Dkt Ruto pia ameivunja Katiba, ambayo aliapa kuitetea.

Ikiwa BBI ingepita, hatungekuwa na kibarua kinachotukabili kwa sasa—tishio za maandamano kutoka kwa kiongozi [asiye rasmi] wa Upinzani, Bw Raila Odinga.

Sababu ya kumnukuu Bw Odinga kama kiongozi asiye rasmi wa upinzani ni kuwa, hana afisi maalum inayotambulika kikatiba anayopaswa kuendeshea shughuli zake kama Kiongozi Rasmi wa Upinzani.

BBI ilipendekeza uwepo wa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani, anayefadhiliwa na serikali. Nafasi hiyo ilikuwepo katika Katiba ya zamani.

Hilo ndilo lililowawezesha viongozi kama Rais Mstaafu (marehemu) Mwai Kibaki, Bw Kenyatta kati ya wengine kuendesha majukumu yao kama viongozi wa upinzani bila matatizo yoyote.

Bw Kibaki alihudumu kama Kiongozi wa Upinzani wakati wa uongozi wa marehemu Daniel Moi, huku Bw Kenyatta akihudumu katika nafasi hiyo kati ya 2002 na 2007, wakati wa muhula wa kwanza wa utawala wa Bw Kibaki.

Ukweli ni kuwa, tunapasa kufufua upya BBI na kuchukua mapendekezo mazuri ambayo yangetufaa, kama vile uwepo wa afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani.

Bila afisi hiyo na ufadhili ufaao kutoka kwa serikali, itakuwa vigumu kwa Bw Odinga na washirika wake kutekeleza majukumu ya upinzani ifaavyo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wawili wakana kumvua nguo mhasiriwa wa wizi wa mabavu

CECIL ODONGO: Uhuru kama mwenyekiti azungumzie siasa na...

T L