• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
WANDERI KAMAU: Uhuru amwige Suluhu ili kulainisha serikali yake

WANDERI KAMAU: Uhuru amwige Suluhu ili kulainisha serikali yake

Na WANDERI KAMAU

MAJUZI, Rais Samia Suluhu wa Tanzania aliwashangaza wengi kwa kuwafuta kazi mawaziri maarufu na wenye ushawishi mkubwa, wengi wakiwa washirika wa karibu wa mtangulizi wake, marehemu John Magufuli.

Kwenye hatua hiyo iliyozua gumzo katika majukwaa mbalimbali nchini humo na eneo nzima la Afrika Mashariki, Rais Samia alisema hatua yake inalenga “kuwapa uhuru wale wanaolenga kuwania nyadhifa za kisiasa kwenye uchaguzi mkuu wa 2025 muda wa kutosha kufanya kampeni zao.”

Bila shaka, huo ulikuwa ujumbe mzito sana wa kisiasa kutoka kwa kiongozi huyo kwa dunia nzima: Yeye si limbukeni tena uongozini kama alivyochukuliwa na wengi katika siku za mwanzo mwanzo.

Ni ujumbe pia unaoashiria kuwa ni kiongozi mwenye uwezo wa kufanya maamuzi huru yanayomfaa na yanayoifaa serikali yake, ili kuwatimizia Watanzania ahadi walizotoa pamoja na Dkt Magufuli.

Ikiwa imebaki miaka mitatu kabla ya uchaguzi huo kufanyika, kile kimejitokeza ni kuwa Rais Suluhu hana nafasi yoyote kuwavumilia watu wanaoendeleza mipango yao ya kisiasa kwa kutumia nafasi walizo nazo serikalini.

Ni wazi hii ni changamoto kubwa kwa Rais Uhuru Kenyatta; kwamba imefikia wakati ailainishe serikali yake, kwa kuwaondoa mawaziri, manaibu wao, makatibu wa wizara, wenyeviti wa idara muhimu kati ya wengine ambao wanaendelea kufanya kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti kwa kutumia raslimali za serikali na nyadhifa wanazoshikilia.

Ingawa sheria inasema maafisa wa serikali wanaolenga kuwania nyadhifa za kisiasa wanapaswa kujiuzulu kutoka nafasi zao miezi sita kabla ya uchaguzi kufanyika, baadhi yao walianza kampeni zao tangu mwaka 2021.

Rais Kenyatta amwige Rais Suluhu kwa kuwaondoa maafisa wanaofanya kampeni wakiwa bado serikalini bila kuogopa lolote.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

UDAKU: Kipendacho roho ya Rashford ni Lucia tu!

TAHARIRI: Tujikaze tufuzu kwa fainali za Dunia, Bara

T L