• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
WANDERI KAMAU: Unga: Serikali imewasaliti raia kwa mfumuko wa bei

WANDERI KAMAU: Unga: Serikali imewasaliti raia kwa mfumuko wa bei

NA WANDERI KAMAU

SERIKALI imewasaliti Wakenya.

Ni kana kwamba haijali maslahi na vilio vyao, hasa kutokana na gharama ya juu ya maisha.

Kiafrika, mzazi anafaa kumsikiliza mwanawe anapolilia au anapolalamikia jambo fulani.

Anafaa kufanya mazungumzo naye ili kufahamu yale yanayomsumbua na kubuni mkakati wa kumsaidia kutatua tatizo hilo.

Hata hivyo, serikali inaonekana kupuuza vilio vya Wakenya, hasa kutokana na bei ya juu ya unga wa mahindi.

Alhamisi wiki iliyopita, Waziri wa Kilimo, Bw Peter Munya, alitangaza kupunguza bei ya unga wa mahindi kwa Sh2, baada ya maelfu ya Wakenya kulalamikia bei za juu za bidhaa hiyo.

Kwa mara ya kwanza tangu uhuru, bei ya pakiti ya kilo mbili ya unga ilipita Sh200.

Kiwastani, kiwango hicho cha unga kinauzwa kati ya Sh200 na Sh240 katika sehemu tofauti nchini.

Bw Munya alieleza kuwa serikali itapunguza bei ya unga ili kuwarahisishia mzigo mamilioni ya Wakenya wanaotegemea bidhaa hiyo kulisha familia zao, wengi walionekana kuwa na matumaini mapya. Hata hivyo, alipotangaza kuwa bei hiyo itapunguzwa kwa Sh2 pekee, wengi walionyesha ghadhbu, wakisema hilo halitawasaidia kwa vyovyote vile.

Wengine walitaja hilo kama “dharau” na “mapuuza ya wazi”.

Wengine pia walisema haingefaa serikali kutangaza mkakati wa kupunguza bei hizo, ila ingeacha bei hizo kubaki zilivyokuwa.

Kuutia msumari kwenye kidonda, Bw Munya alinukuliwa ‘akiwashauri’ Wakenya kuwa mbali na mahindi, wanaweza kutumia vyakula vingine kama mihogo, viazi vikuu, viazi vitamu na vinginevyo.

Bila shaka, hayo si matamshi ya kuridhisha kutoka kwa waziri ambaye anaangaliwa na mamilioni ya Wakenya kuwapa suluhisho kwa changamoto zinazowakumba. Ni kama baba anayewapuuza wanawe licha ya kumlilia awasaidie kuwapa chakula.

Tangu mwaka wa 2002, imekuwa kawaida bei ya unga na bidhaa nyingine za msingi kupanda kupita kiasi kila uchaguzi mkuu unapokaribia.

Hali hiyo ilishuhudiwa katika miaka ya 2007, 2013, 2017 na sasa 2022. Maswali ambayo yamekuwa yakiibuka ni kuhusu wale ambao hupanga njama za kupandisha bei hizo, na sababu yao kutochukuliwa hatua na serikali ambazo huwa mamlakani.

Baadhi ya wanauchumi wamekuwa wakilaumu msingi wetu wa kiuchumi kuwa sababu kuu ya hali hiyo.

Kwa kawaida, msingi wetu wa kisiasa, kiuchumi na kijamii ni wa mfumo wa kibepari. Ni mfumo tuliourithi kutoka kwa mataifa ya Ulaya kama vile Uingereza.

Ingawa huenda hilo ni moja ya sababu ambazo zimekuwa zikitolewa kama kiini kikuu cha tatizo hilo, ni wakati mwafaka kwa serikali kuzinduka na kukoma kupuuza changamoto zinazowakumba mamilioni ya raia.

Wiki iliyopita, kuliibuka ripoti kuhusu vijana kadhaa waliopatikana wakichoma nyama ya mbwa katika eneo la Molo, Kaunti ya Nakuru, wakitaja bei za juu za vyakula kuwasukuma katika ulaji wa mmbwa. Ili kuepuka visa kama hivyo, ni wakati serikali ibuni tatizo la kudumu kuhakikisha raia hawateseki kutokana na ukosefu wa chakula.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Rais hebu sema neno moja tu, bei ya unga ishuke

BENSON MATHEKA: Manifesto hazifai kupandisha joto la...

T L