• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
TAHARIRI: Rais hebu sema neno moja tu, bei ya unga ishuke

TAHARIRI: Rais hebu sema neno moja tu, bei ya unga ishuke

NA MHARIRI

KATIKA siku za hivi karibuni viongozi mbalimbali wakiwemo wa kisiasa na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu, wamekuwa wakiwashauri Wakenya kususia uchaguzi wa Agosti 9 ikiwa serikali haitapunguza bei ya unga.

Serikali inafaa kuchukulia wito huo kwa uzito kwani unaweza kuchochea maandamano kote nchini.

Hali kama hiyo inaweza kuvuruga uthabiti wa nchi wakati huu taifa hili linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wenye ushindani mkuu haswa katika kinyang’anyiro cha urais.

Uzito wa suala hilo kwa taifa la Kenya kwa jumla umedhihiri katika ripoti ya hivi punde inayoonyesha kuwa zaidi ya Wakenya milioni 4.1 wanahitaji chakula cha msaada kwa dharura.

Ama kwa hakika hii ni idadi kubwa zaidi ya raia ambao shida zao znafaa kushughulikiwa haraka kwani ni wajibu wa serikali kuu ni kuhakikisha hamna mwananchi anayekufa kwa njaa.

Serikali isipuuze malalamishi ya viongozi hao kuhusu unga ghali za ajira kwa vijana.

Mbali na kupunguza bei ya unga na bidhaa nyingine za kimsingi, pia wanasiasa hasa wanaowania viti vya urais wanapaswa kumakinika ili wakiingia mamlakani, hali kama hii isitokee tena.

Katika manifesto nyingi ambazo viongozi hao wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto na kinara wa ODM, Raila Odinga, suala la kilimo limepewa umuhimu.

Naam, kilimo kikitiliwa mkazo inavyofaa, hali kama hii haiwezi kutokea.

Lakini nyingi ya manifesto hizi hupuuzwa pindi kura zinapopigwa.

Kwa mfano, Serikali ya Jubilee ambayo iko chini ya Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto, imefeli pakubwa hasa katika kutimiza ahadi ilizotoa kabla ya kuingia mamlakani.

Baadhi ya ahadi hizo maarufu ni kama vile utoaji wa laptopu kwa wanafunzi wote wanaoingia darasa la kwanza, ujenzi wa viwanja vitano vya hadhi ya kimataifa pamoja na ujenzi wa makazi ya bei nafuu ili kuwaondolea wakazi wa mijini kero la kulipa kodi.

Ila, hayo sasa, walivyosema wahenga, ni sawa na yaliyopita ambayo si ndwele. Muhimu ni kuganga yajayo katika muktadha wa kuhakikisha ahadi zilizotolewa mara hii zinatekelezwa zote bila kukosa.

Wawaniaji wakuu wa urais wamedai kuwa wameshauriwa kwa mapana na wataalamu wa kiuchumi kabla ya kutoa manifesto zao.

Kwa hivyo, ni matarajio ya wengi kuwa hawatatoa vijisababu vya kutotekeleza ahadi hizo mara hii.

You can share this post!

Jumwa ahepa tena mjadala uliogeuka wa kukosoa Kingi

WANDERI KAMAU: Unga: Serikali imewasaliti raia kwa mfumuko...

T L