• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
WANDERI KAMAU: Wanaume Afrika wafuate nyayo za  Wazungu kuwakweza akina mama

WANDERI KAMAU: Wanaume Afrika wafuate nyayo za Wazungu kuwakweza akina mama

Na WANDERI KAMAU

KATIKA jamii nyingi za Kiafrika, wanaume huchukulia wanawake kama viumbe dhaifu wasioweza chochote.

Baadhi hata huwaona kama binadamu wasiofaa kuwepo duniani.

Ni kutokana na kasumba hizo ambapo wanaume wengine huwadharau sana wanawake, kiasi cha kushikilia kuwa hawana usemi wowote kwenye masuala muhimu kama urithi na masuala ya kitamaduni.

Wengine hata huendeleza tamaduni za kikale kuwa wanawake hawapaswi kusoma au kujitosa kwenye ulingo wa siasa. Hata hivyo, mdahalo kuhusu nafasi halisi ya mwanamke katika jamii uliibuka upya Jumamosi, kufuatia ushujaa wa kipekee uliodhihirishwa na rubani Ruth Karauri wa Shirika la Ndege la Kenya (Kenya Airways).

Bi Karauri alisifiwa kila pembe ya dunia, baada ya kuhimili makali ya kimbunga Eunice nchini Uingereza, kwa kutua kishujaa katika Uwanja wa Ndege wa Heathrow jijini London, wakati marubani wengine walishindwa kufanya hivyo.

Bi Karauri alikuwa akiendesha ndege aina ya Boeing 787 kwa ushirikiano na rubani Clive Nyachieo.

Baada ya kusifiwa katika majukwaa na kumbi za majadiliano katika vyombo vya habari na mitandaoni, Bi Karauri alimsifia mumewe kuwa “sehemu ya mafanikio yake.” Mumewe Bi Karauri ni Bw Ronald Karauri, ambaye ndiye Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya SportPesa. Bw Karauri analenga kuwania ubunge katika eneo la Kasarani, Nairobi.

Akirejelea ufanisi wa mkewe, Bw Karauri aliwashauri wanaume kutoogopa kuwasaidia wake zao kufanikisha ndoto walizo nazo maishani katika kila fani.

“Msiogope ushindani kutoka kwa wake zenu. Badala yake, wajengeni ili waweze kutimiza matamanio yao maishani. Ufanisi wao utakuwa wenu nyote wawili,” akashauri Bw Karauri.

Bila shaka, ushauri huo unapaswa kuwa changamoto kwa wanaume, kwamba nyakati zimebadilika.

Tunaishi katika nyakati ambapo baadhi ya tamaduni hazina nafasi yoyote katika jamii na maisha ya kisasa.

Tamaduni kama ndoa za mapema na za kulazimishwa zimepitwa na wakati. Wanawake ni binadamu ambao kinyume na dhana za kikale, wana uwezo, werevu na haki sawa na wanaume.

Ingawa Waafrika huwa na mazoea ya kuwakosoa Wazungu kutokana na tamaduni zao “potovu”, wanapaswa kuwaiga kwa mtindo wao wa kuwapa nafasi wanawake wao katika karibu kila nyanja.

Kwa mfano, asili ya baadhi ya viongozi wanawake wenye sifa na ushawishi mkubwa zaidi duniani ni Amerika na Ulaya.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Walimu wasihujumu mitihani ya kitaifa wakitafuta...

LEONARD ONYANGO: Malumbano baina ya wanasiasa hayatasaidia...

T L