• Nairobi
  • Last Updated September 26th, 2023 10:25 PM
WANDERI KAMAU: Wito kwa Rais William Ruto; waondoe mawaziri wazembe!

WANDERI KAMAU: Wito kwa Rais William Ruto; waondoe mawaziri wazembe!

NA WANDERI KAMAU

KUNA ukimya mkuu uliotanda kila sehemu nchini. Ukimya mkubwa!

Ukimya ambao unaifanya vigumu kuamini ikiwa kuna serikali inayoongoza nchi au la.

Ingawa wahenga walisema kuwa watu wangwana mara nyingi huwa hawazungumzi, ukimya uliopo unatisha, unasikitisha na kuatua moyo!

Nazungumzia ukimya wa mawaziri wa Rais William Ruto. Hawasikiki hata kidogo!

Matamshi tunayoyasikia tu ni ya Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua wakijibu vigogo wa Azimio kuhusu vile “waliwashinda” kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2023.

Kwa Bw Gachagua, yamekuwa mazoea kwake kurejelea kiongozi wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga, na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kuhusu vile waliwashinda debeni licha yao kuwa serikalini.

Mtindo uo huo ndio amekuwa akiiga Dkt Ruto, kwa kusisitiza kuwa wataendelea kuwafanyia Wakenya kazi bila kujali “kelele kutoka upinzani”.

Pengine kiongozi ambaye ameonyesha utofauti fulani katika utendakazi wake ni Kinara wa Mawaziri, Bw Musalia Mudavadi.

Huyu amekuwa akiendesha majukumu yake kimya kimya bila kutoa matamshi kanganyishi.

Ijapokuwa si lazima mawaziri wasikike wanapofanya kazi, ukimya uliopo unazua wasiwasi kuhusu ikiwa kweli wanadhibiti wizara zao.

Kwa mfano, kulingana na ripoti iliyotolewa juzi na shirika la utafiti wa kura za maoni la Infotrak, hakuna waziri hata mmoja alifikisha asilimia 50 katika utendakazi wake. Wote walipata chini ya asilimia 30.

Kinaya ni kuwa, Profesa Kithure Kindiki ndiye aliyeorodheshwa wa kwanza miongoni mwa mawaziri; ila anaonekana kushindwa kuidhibiti Wizara ya Usalama wa Ndani kutokana na visa vya mauaji na wizi wa mifugo, ambavyo vimekuwa vikiendelea katika eneo la Bonde la Ufa.

Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu aliorodheshwa wa pili. Naye pia anaonekana kushindwa kabisa kuidhibiti wizara hiyo, ikilinganishwa na mtangulizi wak marehemu George Magoha.

Katika kipindi cha mwezi mmoja sasa masomo hayajaendelea katika shuleni nyingi za umma za Sekondari ya Msingi (JSS), kutokana na ukosefu wa walimu na miundomsingi ya kutosha.

Wazazi wengi wameamua kurejesha wanawao darasa la nane ili wafanye mtihani wa kitaifa (KCPE) kuepuka mkwamo huo.

Katika Wizara ya Utalii, Waziri Peninah Malonza hasikiki.

Katika Wizara ya Afya, hatujamwona Waziri Susan Nakhumincha akizungumzia masuala muhimu, kama vile mkurupuko wa kolera ambao umeripotiwa katika kaunti za Kiambu na Nairobi.

Mawaziri wengine pia wako kimya hawaonekani kuelewa majukumu yao, huku raia wakiteseka.

Rais Ruto tafadhali wabadilishe mawaziri wako. Lifanyie mageuzi baraza lako la mawaziri.

Yawezekana kuwa ni mapema sana kufanya mageuzi, lakini wananchi hawahisi utendakazi wao wowote.

Ili kujiokoa mapema dhidi ya ghadhabu za raia, tafadhali waondoe mawaziri ambao hadi sasa hawaonekani kuelewa majukumu yao.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Safari ya kisiasa ya Harrison Kombe ambaye mahakama imefuta...

Ndugu waagizwa wamalize kesi nje ya korti

T L