• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
WANTO WARUI: Serikali iendelee kutatua changamoto zinazokabili sekondari msingi nchini

WANTO WARUI: Serikali iendelee kutatua changamoto zinazokabili sekondari msingi nchini

NA WANTO WARUI

MAJUMA matatu sasa tangu shule za sekondari msingi kuanza mafunzo yake,bado shule nyingi hazijaweka mikakati bora ya kuendeleza ufunzaji wake.

Shule nyingi za umma zingali katika ndoto ya kupata walimu wa kufunza masomo yanayohitajika huku Tume ya Huduma za Walimu (TSC) ikituma mwalimu mmoja tu au wawili katika kila shule. Hii ni kinyume na ahadi iliyotolewa na serikali kuwa shule za sekondari msingi zitakuwa na walimu wa kutosha.

Katika shule nyingi za umma, wanafunzi wamefurika madarasani kutokana na hali mbaya ya kiuchumi ambayo imesababisha wazazi wengi kuhamisha watoto wao kutoka shule za kibinafsi.

Madarasa yana wanafunzi wengi huku idadi ikiwa 80 au 90 kutokana na ongezeko hilo. Katika hali kama hii, walimu wanaotegemewa kufunza wanafunzi hawa wa Gredi ya 7 wanajipata pabaya kwani hawatoshi kabisa. Kuna baadhi ya shule ambako mwalimu mmoja analazimika kufunza masomo matano.

Kutokana na uhaba huu wa walimu, walimu wakuu wa shule za msingi, ambao pia ndio wanaosimamia sekondari msingi, wanajipata wakijumlisha walimu wa shule za msingi katika mpango wote wa kufundisha Gredi ya 7.

Iwapo walimu hawa hawataweza kuongozwa vyema, basi kutakuwa na tatizo kubwa katika utekelezaji wa mafunzo ya sekondari msingi. Hakuna shaka hatua za dharura zinafaa kuchukuliwa ili kuokoa hali hii.

Uhaba wa vifaa vya masomo kama vile maabara, karakana za masomo ya sanaa, ni kizingiti kikubwa cha masomo katika shule nyingi.

Iwapo serikali haitaingilia kati ili kuokoa hali hizi, basi wanafunzi wa Gredi 7 watatatizika sana na kubaki nyuma kimasomo kulingana na mahitaji ya mtaala huu wa masomo ya CBC.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Ungependa kukumbukwa vipi utakapoondoka...

9 wauawa katika vita Somaliland

T L