• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
AFC Leopards yapokonya Mukangula na Thiong’o majukumu ya unahodha baada ya mgomo baridi

AFC Leopards yapokonya Mukangula na Thiong’o majukumu ya unahodha baada ya mgomo baridi

NA JOHN ASHIHUNDU

KLABU ya AFC Leopards imewapokonya mamlaka manahodha wake Eugene Mukangula na Peter Thiong’o.

Taarifa ya klabu hiyo imesema hatua hiyo ya kinidhamu imechukuliwa kufuatia mgomo baridi uliofanywa na wachezaji wa timu hiyo mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na Taifa Leo mnamo Jumatano, mwenyekiti wa klabu hiyo Dan Shikanda alisema wachezaji walikataa kufanya mazoezi na kuendesha shughuli zao polepole kama ishara ya kugoma ili kushinikiza afisi iwamalizie asilimia 25 ya mshahara wao wa mwezi Mei – kiasi ambacho kilikuwa kimebakia.

Leopards walifanya mgomo huo wakati timu ilikuwa ikijiandaa kwenda Kakamega kucheza na Vihiga Bullets katika mechi ya Ligi Kuu ya Kitaifa mjini Mumias, mechi ambayo baadaye walienda na kuchapwa 2-1 na klabu hiyo ambayo tayari imeshuka hadi daraja la Supa Ligi (NSL).

“Kama kamati kuu ya klabu, tumechukua hatua hii kuambatana na sheria zetu. Wachezaji walitenda kinyume cha sheria, kwani tulikuwa tumekubaliana wasubiri hadi Jumanne tuwalipe pesa zilizobakia, lakini wakaamua kuharakisha mambo. Hii ni aibu kwa wadhamini wetu ambao wamekuwa wakiwalipa kwa wakati ufaao,” amesema Bw Shikanda.

Akaongeza: “Wadhamini wetu, Betika, wamekuwa wakilipa wachezaji bila kuchelewa. Tuliwaambia wasubiri tuwajazie pesa zilizobakia mapema wiki hii, lakini tulishangazwa na jinsi walivyoamua kufanya mgomo baridi.”

Mukangula aliteuliwa kuwa nahodha mkuu wa Leopards mnamo Aprili 2022 kujaza nafasi ya Marvin Nabwire aliyeondoka na kujiunga na Kenya Police FC, wakati Thiong’o akiteuliwa kuwa naibu wake.

Lakini hata baada ya hatua hiyo kuchukuliwa, mashabiki wa klabu hiyo wametoa maombi tofauti ya kupongeza afisi kutokana na adhabu hiyo, huku wengine wakiishutumu afisi ya Shikanda kwa kuadhibu wachezaji hao waliouliza haki yao.

Lakini akitetea afisi yake, Shikanda alisema Mukangula na Thiong’o walishindwa kutekeleza wajibu wake kama viongozi na badala yake wakachochea wenzake kuendeleza kutoa vitisha kwa afisi.

“Wachezaji walikataa kuingia kwa basi kuanza safari wakisisitiza lazima walipwe pesa zao kwanza. Tulitarajia Mukangula na Thiong’o kushawishi wenzao wakubali kucheza, lakini wakashindwa. Kwa kushindwa kushawishi wenzao, manahodha hao wameharibu jina la timu na kutoa picha mbaya mbele ya wadhamini wetu Betika,” aliongeza huku akisema kamati yake imempa kocha Patrick Aussems idhini ya kutafuta wachezaji wa kujaza nafasi hizo mbili.

“Awali tulikuwa na shida nyingi chini ya nahodha Robinson Kamura, lakini hatukushuhudia haya. Matumizi yetu ya kifedha kwa mwezi mmoja ni Sh4.2 milioni, na kuna wakati tunalemewa kuwalipa marupurupu kwa wakati, lakini hawafai kufikisha pale wamefika, ikikumbukwa kwamba hali yetu ya kifedha sio nzuri.”

  • Tags

You can share this post!

Mfanyabiashara ashtakiwa kwa wizi wa mbolea ya Sh6 milioni

Mishahara ya wabunge yachelewa tena

T L