• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:55 AM
AFC: Wasiwasi kambini kuhusu kocha Aussems

AFC: Wasiwasi kambini kuhusu kocha Aussems

Na JOHN ASHIHUNDU

KLABU ya AFC Leopards imekumbwa na wasiwasi baada ya kocha Patrick Aussems kuondoka nchini, kufuatia marufuku ya serikali iliyositisha tena michezo ili kudhibiti wimbi la tatu la virusi vya corona.

Mbelgiji huyo mwenye umri wa miaka 56 aliondoka baada ya Rais Uhuru Kenyattta kutangaza marufuku hayo kwa muda wa siku 21.

Ligi za soka nchini ni miongoni mwa shughuli zote za michezo zilizopigwa marufuku Rais alipotoa marufuku mpya ya kuingia na kutoka katika miji mitano iliyoathiriwa pakubwa na maambukizi ya corona.

Aussems ni miongoni mwa makocha walioamua kurudi nyumbani ili kuwa karibu na familia zao wakati ambapo marufuku inatekelezwa, lakini hajawasiliana na wajiri wake AFC Leopards kuhusu hatima yake ya baadaye klabuni.

“Kutokana na marufuku nimeamua kwenda nyumbani kutembelea jamii yangu nikisubiri michezo kurejelewa,” alisema Aussems kabla kuondoka.

“Bila shaka nitarejea hali itakaporudi kama kawaida. Jihadharini na mfuate maagizo ya Wizara ya Afya wakati huu mgumu. Nawatakieni Pasaka njema mashabiki wote wa soka.”

Majuzi, rais wa FKF , Nick Mwendwa aliwahakikishia Wakenya kwamba mazungumzo yanaendelea baina yao na Wizara ya Michezo kwa lengo la kurejesha soka.

“Tayari tumezungmza na Wizara ya Michezo, na wako tayari kurekebisha mambo fulani. Wanataka tuandike barua kuahidi kwamba tuko tayari kufuata maagizo yaliyowekwa kudhibiti corona.

“Kadhalika tumeeleza Waziri Amina Mohamed kuhusuu athari za marufuku hii kwa klabu zetu pamoja na timu ya taifa Harambee Stars, ambayo mwezi Juni itakuwa uwanjani kucheza mechi ya kufuzu Kombe la Dunia,” alitanguliza.

Aliongeza Nick Mwendwa: “Naweza sema kuwa Bi Amina yuko tayari kutukubalia turejelee soka, iwapo tu tutafuata maagizo ya Wizara ya Afya kuhusu vita dhidi ya Covid-19. Tunasubiri jibu kwa barua yetu tukitarajia mema.”

Ligi za FKF zimekuwa zikiendelea kwa miezi mitano pasipo mashabiki viwanjani, huku wachezaji wakifanyiwa vipimo mara kwa mara, mbali na viwanja kunyunyuziwa dawa ya kuangamiza virusi vya corona.

 

You can share this post!

PATA USHAURI WA DKT FLO: Nitakabili vipi ‘allergy’ ya...

Liverpool kucheza dhidi ya Real Madrid leo usiku