• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
AFCON: Wanahabari watatu wa Algeria wavamiwa na wahalifu nje ya hoteli nchini Cameroon

AFCON: Wanahabari watatu wa Algeria wavamiwa na wahalifu nje ya hoteli nchini Cameroon

Na MASHIRIKA

WANAHABARI wa Algeria walivamiwa ka visu jijini Douala katika siku ya ufunguzi wa kampeni za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon.

Mehdi Dahak anayemiliki tovuti moja ya soka nchini Algeria amesema mwanahabari mwenzake alijipata katika ulazima wa kutibiwa hospitalini baada ya kukatwa vibaya mara mbili naye akijeruhiwa usoni.

Tukio hilo la Jumapili usiku lilishuhudia pesa, simu tatu za mkononi na pasipoti za wanahabari watatu zikiibwa sekunde chache tu baada yao kutoka nje ya hoteli yao katika eneo la Bonapriso, jijini Yaounde, Cameroon.

Maafisa wa usalama wameanzisha uchunguzi huku balozi wa Algeria nchini Cameroon akihimiza uchunguzi huo ufanywe haraka iwezekanavyo.

Licha ya kujeruhiwa, Dahak na wenzake wameapa kuendelea kuangazia michuano ya makala ya 33 ya fainali za AFCON mwaka huu. Kipute hicho kilikuwa kifanyike mnamo 2021 ila kikacheleweshwa kutokana na janga la corona.

“Mwenzangu alichomwa kisu mara mbili mgongoni. Alipelekewa hospitali ambapo majeraha hayo yalishonwa. Kwa sasa anapata nafuu na ana hamu ya kuendelea kuangazia matukio ya fainali hizi hapa Cameroon. Tulivamiwa karibu mita 10 tu nje ya hoteli,” akasema Dahak.

Kwa mujibu wa Dahak, wahalifu wao walikuwa wakiwasubiri kwa muda mrefu nje ya hoteli hiyo.

Mwanahabari Smail Mohamed Amokrane ndiye aliumia vibaya huku mwingine akiponea chupuchupu baada ya kurejea ndani ya hoteli harakaharaka wenzake walipovamiwa nje.

Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) limesema linashirikiana na mamlaka husika ya usalama nchini Cameroon kuchunguza kisa hicho huku Serikali ya Cameroon ikiahidi kuimarisha usalama katika eneo la Limbe, Kusini Magharibi mwa Cameroon, litakalokuwa mwenyeji wa mechi nane za AFCON.

Cameroon ambao ni mabingwa mara tano wa AFCON wanakuwa wenyeji wa kipute hicho kwa mara ya kwanza baada ya miaka 50. Fainali ya kipute hicho itafanyika jijini Yaounde mnamo Februari 6, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Ruto na Raila wakanye wandani wao kuchochea

Madaktari 10 wa Mombasa kufaidika kwa mafunzo zaidi nchini...

T L