• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
CHARLES WASONGA: Ruto na Raila wakanye wandani wao kuchochea

CHARLES WASONGA: Ruto na Raila wakanye wandani wao kuchochea

Na CHARLES WASONGA

MAANA ya msemo, ‘Nyani haoni kundule, huona la mwenzake’ ilidhihirika mnamo wikendi baada ya kukamatwa kwa Seneta wa Meru Mithika Linturi kwa tuhuma za kutumia maneno ya kuchochea chuki katika mkutano wa kisiasa mjini Eldoret.

Hii ni baada ya wanasiasa wa mrengo wa Azimio la Umoja, wakiongozwa na kinara wao, Raila Odinga kumwelekezea Bw Linturi mishale ya lawama, kwa misingi kuwa matamshi yake yanaweza kusababisha vita na uhasama kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Sisemi kwamba Bw Odinga na wandani wake hawakupaswa kulaani matamshi ya mwanasiasa huyo. La hasha!

Ni haki yao kama Wakenya kulaani matamshi ambayo yanaweza kuvuruga amani na uthabiti wa kisiasa nchini.

Ama kwa hakika amri ya kukamatwa kwa Seneta Linturi iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noodin Haji ilichochewa na malalamishi ya Wakenya mitandaoni.

Huku Bw Odinga, Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi nchini (COTU) Francis Atwoli, na wanasiasa wengine wanaoegemea mrengo wa Azimio, wanapomkashifu Bw Linturi wakumbuke kuwa ndani ya kambi yao pia kuna wachochezi.

Wakenya wanaofuatilia habari kwenye mitandao ya kijamii, walimkumbusha Bw Odinga na wenzake visa kadhaa ambapo wandani wake wamewahi kuchochea chuki na kukamatwa na polisi.

Kwa mfano mnamo 2016, wandani wa Bw Odinga; wabunge Junet Muhamed (Suna Mashariki), Florence Mutua (Mwakilishe wa Kike wa Busia) na Johnson Muthama (aliyekuwa Seneta wa Machakos) walikamatwa kwa kutoa matamshi ya chuki

Isitoshe, mwaka jana, baadhi ya wanasiasa wanaounga mkono ndoto ya Bw Odinga ya kuingia Ikulu mwaka huu wamewahi kutumia maneno yale yale ambayo Seneta Linturi alitumia Eldoret, Jumamosi.

Ingawa wanasiasa hao hawakuchukuliwa hatua zozote za kisheria, ikumbukwe kwamba maneno kama vile “madoadoa” na “kwekwe” ni mojawapo ya vichochezi vya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.

Kile Bw Odinga na Naibu Rais William Ruto wanafaa kufanya wakati kama huu ni kuwadhibiti washiriki wao dhidi ya kutoa matamshi ya kuchochea chuki na uhasama wa aina yoyote ile, taifa hili linapoelekea katika uchaguzi mkuu.

Ninaamini kwamba wawili hao, ambao ni wagombeaji urais wenye ushawishi mkubwa nchini, wana uwezo wa kufanya hivyo.

Kwa mfano, duru zinaarifu kwamba kabla ya mkutano wa Jumamosi katika uwanja wa Eldoret Club, Dkt Ruto alifanya mkutano na karibu viongozi 100 wanaoegemea chama chake cha United Democratic (UDA) nyumbani kwake Sugoi.

Nadhani ni katika mkutano kama huo ambapo Dkt Ruto alipanga orodha ya wabunge ambao walipaswa kuhutubia katika mkutano huo, ambapo mwanasiasa huyo alipewa baraka za wakazi anapowania urais.

Ni katika mkutano, ambapo Dkt Ruto alipaswa kuwashauri wanasiasa hao kuhusu yale wanapaswa kusema na yale hafai kutamka.

Kwa upande, mwingine Bw Odinga pia anaweza kufanya hivyo katika mikutano yake ya kujipigia debe kote nchini.

Ukweli ni kwamba, nilivyotaja hapa, kuna baadhi ya wandani wa Bw Odinga wenye ndimu za sumu.

Kwa hivyo, iwapo Dkt Ruto na Bw Odinga wanataka kuongoza taifa lenye amani na umoja baada ya uchaguzi wa mwaka huu, basi hawana budi kuwadhibiti wandani wao.

  • Tags

You can share this post!

JUMA NAMLOLA: Ababu angefanyia haya rais mwengine, angekuwa...

AFCON: Wanahabari watatu wa Algeria wavamiwa na wahalifu...

T L