• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Arsenal kwenye mizani

Arsenal kwenye mizani

Na MASHIRIKA

FATAKI zitalipuka na nyasi kuumia leo ugani Goodison Park wakati Everton watashuka dimbani kuvaana na Arsenal katika pambano kali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Sawa na Arsenal waliotandikwa 3-2 na Manchester United katika mechi ya awali ligini, Everton watakuwa pia wakiwinda fursa ya kujinyanyua baada ya Liverpool kuwacharaza 4-1 kwenye gozi la Merseyside mnamo Jumatano iliyopita.

Kichapo kingine kwa Everton kitazidisha presha ya kupigwa kalamu kwa kocha Rafael Benitez ambaye sasa ameshuhudia waajiri wake wakikosa kushinda mechi yoyote ya EPL kutokana na nane zilizopita.Baada ya kushinda mechi nne, kutoka sare mara tatu na kupoteza michuano saba kati ya 14 hadi kufikia sasa msimu huu, Everton wanajivunia alama 15 zinazowaweka katika nafasi ya 15 jedwalini.

Ni pengo la pointi nane ndilo linatamalaki kati yao na Arsenal ambao wameongoza na mkufunzi Mikel Arteta kushinda mechi saba na kuambulia sare mara mbili baada ya michuano 14 ligini muhula huu.Licha ya kuanza vyema kampeni za msimu huu, Everton wamepoteza mechi sita kati ya nane zilizopita ligini.

Kikosi hicho kimefungwa mabao manane nacho kikapachika wavuni goli moja pekee kutokana na mechi tatu zilizopita ambazo kimepoteza kwa mfululizo.Ingawa jeraha linalouguzwa na fowadi Dominic Calvert-Lewin linahusishwa pakubwa na masaibu ya Everton, uthabiti wa klabu hiyo katika safu zote umeshuka na hali hiyo inatarajiwa kuchangia motisha zaidi ya Arsenal.

Ushindi kwa Arsenal utaendeleza rekodi duni ya Everton ambao watakuwa wamepoteza mechi nne kati ya tano zilizopita katika uwanja wao wa nyumbani.Mechi ya Alhamisi iliyopita ilishuhudia rekodi ya Arsenal ya kutopoteza mechi sita dhidi ya Man-United ligini ikipigwa breki kali ugani Old Trafford.

Aidha, masogora wa Arteta walipoteza fursa nzuri ya kuwaruka West Ham United na kuingia ndani ya mduara wa nne-bora jedwalini.Sasa ni pengo la pointi nne ndilo linatenganisha Arsenal na nambari nne West Ham walioduwaza Chelsea kwa kichapo cha 3-2 mnamo Jumamosi ugani London.

Mabingwa watetezi Manchester City walitua kileleni mwa jedwali kwa mara ya kwanza muhula huu baada ya kupepeta Watford 3-1. Liverpool walipaa hadi nambari mbili baada ya kulaza Wolves 1-0.Iwapo Arsenal watazidiwa ujanja, basi itakuwa mara yao ya tatu mfululizo kupoteza mechi wanayoisakata ligini usiku wa Jumatatu na waliwahi kuweka rekodi hiyo mnamo Februari 2019.

Ingawa Arsenal wanapigiwa upatu wa kuzamisha chombo cha wenyeji wao, rekodi yao dhidi ya Everton ni duni. Walitandikwa 2-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza ligini msimu jana ugani Goodison Park kabla ya kupigwa 1-0 katika gozi la marudiano uwanjani Emirates.

Aidha, Arsenal wanajivunia kushinda mechi moja pekee kati ya tano zilizopita dhidi ya Everton ligini.Huku Everton wakikosa huduma za Calvert-Lewin, Tom Davies na Salomon Rondon, Arsenal watakuwa bila Sead Kolasinac, Bernd Leno na Granit Xhaka ambao wauguza majeraha.

You can share this post!

Mourinho pabaya Italia baada ya Roma kuzamishwa tena ligini

Masikitiko Gor ikibanduliwa Caf nyumbani

T L