• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Arsenal waendeleza masaibu ya Man-United katika EPL

Arsenal waendeleza masaibu ya Man-United katika EPL

Na MASHIRIKA

ARSENAL waliweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao baada ya kupepeta Manchester United 3-1 ugani Emirates.

Man-United walishuka dimbani wakilenga kushinda Arsenal nyumbani kwa mara ya kwanza baada ya kulemewa katika mechi tatu mfululizo za awali. Walipigwa 2-0 Machi 2019 kabla ya kupokezwa kichapo sawa na hicho Januari 2020 kisha kuambulia sare tasa Januari mwaka jana.

Arsenal walioshiriki soka ya UEFA mara ya mwisho mnamo 2016-17, sasa wanajivunia alama 60 kutokana na mechi 33 za EPL msimu huu. Pengo la pointi sita linatamalaki kati yao na Man-United wanaokamata nafasi ya sita baada ya kutandaza michuano 34.

Ili kuhimili ushindani mkali katika vita vya kuingia nne-bora, Arsenal wana kibarua kizito cha kuangusha West Ham United katika gozi lijalo kabla ya kumenyana na Spurs na Everton. Spurs waliokuwa wageni wa Brentford mnamo Aprili 23, 2022 nao wana mtihani mgumu dhidi ya Liverpool na Arsenal kabla ya kutamatisha kampeni zao dhidi ya Burnley na Norwich City.

Mabao ya Arsenal dhidi ya Man-United waliofutiwa machozi na Cristiano Ronaldo kabla ya Bruno Fernandes kupoteza penalti katika dakika ya 57, yalipachikwa wavuni kupitia kwa Nuno Tavares, Bukayo Saka na Granit Xhaka.

Ushindi wa Arsenal ulikuwa wa pili chini ya siku nne. Walikomoa Chelsea 4-2 ugenini mnamo Jumatano, siku moja baada ya Man-United kupondwa na Liverpool 4-0 ugani Anfield. Tavares aliwaweka Arsenal kifua mbele baada ya kuchuma nafuu kutokana na masihara ya Raphael Varane na Alex Telles.

Eddie Nketiah alishuhudia bao lake likifutiliwa mbali na teknolojia ya VAR kabla ya Saka kufunga penalti baada ya Telles kumchezea visivyo ndani ya kijisanduku. Kichapo kutoka kwa Arsenal kilididimiza kabisa matumaini finyu ya Man-United kufuzu kwa soka ya UEFA mnamo 2022-23.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mchujo Nandi Hills: UDA yafutilia mbali ushindi wa Alfred...

Shule ya upili ya Shibanga yanasa jicho la Magoha

T L