• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Mchujo Nandi Hills: UDA yafutilia mbali ushindi wa Alfred Keter

Mchujo Nandi Hills: UDA yafutilia mbali ushindi wa Alfred Keter

NA CHARLES WASONGA

CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) chake Naibu Rais William Ruto, kimefutulia mbali ushindi wa mbunge wa Nandi Hillis Alfred Keter katika kura ya mchujo iliyofanyika Aprili 19, 2022.

Hii ni kufuatia rufaa ambayo iliwasilishwa na mwaniaji tiketi hiyo Benard Kitur, aliyeibuka wa pili katika kinyang’anyiro hicho.

Bw Keter, ambaye amekuwa mkosoaji mkuu wa Dkt Ruto, alitangazwa mshindi kwa kuzoa kura 10,363 mbele ya Bw Kitur aliyepata kura 7,468.

Baada ya ushindi huo, Bw Keter alikabidhiwa cheti cha uteuzi cha muda japo baada ya cheti hicho kucheleweshwa kwa zaidi ya saa nane.

Lakini Ijumaa, Aprili 22, 2022, Kamati ya Kusikiza Malalamishi kuhusu Masuala ya Uchaguzi ilifutilia mbali matokeo hayo kufuatia rufaa iliyowasilishwa na Bw Kitur.

Mwaniaji huyo alidai kuwa shughuli hiyo ya kura ya mchujo ilizongwa na visa vya udanganyifu.

Kwa mfano, Bw Kitur alidai kulikuwa na visa vya ambapo masanduku fulani yalipatikana yamejazwa karatasi za kura zilizopigwa na kucheleweshwa kwa uwasilishaji wa matokeo kutoka vituo vya kupigia kura hadi kituo kikuu cha kujumuisha kura.

Kamati hiyo ilikubaliana na madai ya Bw Kitur, ikisema hakukuwa na idadi tosha ya karatasi za kupigia kura katika nyingi za vituo.

Hali hiyo, kamati hiyo ikasema, iliwakosesha wakazi wengi nafasi ya kutekeleza haki yao ya kupiga.

Kamati hiyo ilishangaa ni kwa nini wawaniaji wengine walikubali shughuli hiyo iendelee ilhali hakukuwa na idadi tosha ya karatasi za kupigia kura.

Wawaniaji hao walikuwa ni pamoja na” Robert Chepkwony aliyepata kura 2, 539, Abraham Limo aliyepata kura 540, George Tarus alijishindia kura 425 na Irine Chemtai aliyekuwa wa mwisho kwa kupta kura 388 pekee.

“Makubaliano kwamba shughuli ya upigaji kura uendelee licha ya ukweli kwamba hakukuwa na idadi tosha ya karatasi za kupigia kura, ulifikiwa na wawaniaji. Hatujui mamlaka hii ilitoka wapi. Hatua hii ilikuwa sawa na kuingilia wajibu wa afisa msimamizi wa uchaguzi,” kamati hiyo ilisema katika matokeo ya uchunguzi wake.

“Tumechunguza taarifa zote zilizowasilishwa mbele yetu na pande zote pamoja na ushahidi uliowasilishwa. Tumeshawishika kuwa madia hayo yaliathiri pakubwa matokeo na hivyo kushusha hadhi ya shughuli hiyo,” kamati hiyo ikasema.

Kwa hivyo, kamati hiyo ilifutilia mbali matokeo hayo ya kuwasilisha suala hiyo kwa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ili ifanye uamuzi wake wa mwisho. Hii ni kwa sababu kipindi cha kuandaliwa kwa kura za mchujo kilifikia kikomo Ijumaa.

Akizungumzia uamuzi huo, Bw Keter alisema haelewi ni kwa nini kamati hiyo ilifikia uamuzi huo.

“Nimemwachia Mungu suala hilo ili aingilie kati,” Bw Keter akasema kupitia akaunti yake ya twitter, mnamo Jumamosi, Aprili 23, 2022.

  • Tags

You can share this post!

Timu ya Ruto yaahirisha kampeni Kenya ikiomboleza Kibaki

Arsenal waendeleza masaibu ya Man-United katika EPL

T L