• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Arsenal wakomoa Brentford ugenini na kurejea kileleni mwa jedwali la EPL

Arsenal wakomoa Brentford ugenini na kurejea kileleni mwa jedwali la EPL

NA MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

ARSENAL walikung’uta Brentford 3-0 ugani Gtech Community mnamo Jumapili na kurejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mabao ya kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta yalijazwa kimiani na William Saliba, Gabriel Jesus na sajili mpya, Fabio Vieira.

Ni pambano lililomshuhudia chipukizi Ethan Nwaneri wa Arsenal akiweka rekodi ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa katika EPL akiwa na umri wa miaka 15 na siku 181.

Arsenal sasa wameshinda mechi sita kati ya saba zilizopita za EPL msimu huu na wanajivunia alama 18, moja mbele ya Tottenham Hotspur na mabingwa watetezi, Manchester City. Spurs walipepeta Leicester City 6-2 huku Man-City wakitandika Wolverhampton Wanderers 3-0 mnamo Jumamosi.

Ushindi wa Arsenal unatarajiwa kuwapa motisha ya kukabiliana na mitihani migumu ya Oktoba ambapo watatandaza mechi tisa zikiwemo tano za EPL dhidi ya Spurs, Liverpool, Leeds United, Southampton na Nottingham Forest.

Kikosi hicho kinachowania fursa ya kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao, kwa mara ya kwanza tangu 2016-17, kitamenyana pia na Bodo/Glimt ya Norway na PSV Eindhoven ya Uholanzi katika Europa League mwezi ujao.

Brentford walicharaza Arsenal 2-0 mnamo Agosti 2021 katika pambano lao la kwanza kabisa katika EPL. Hata hivyo, Arsenal walijinyanyua katika mkondo wa pili na kulipiza kisasi kwa ushindi wa 2-1 ugani Emirates.

Matokeo ya Arsenal dhidi ya Brentford yalifuta rekodi yao mbaya ya awali ya kutokamilisha mechi nne mfululizo bila kufungwa bao katika mashindano yote.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ishara Rais kupuuza ahadi kwa washirika

Real wakung’uta Atletico kwenye gozi la La Liga

T L