• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Real wakung’uta Atletico kwenye gozi la La Liga

Real wakung’uta Atletico kwenye gozi la La Liga

Na MASHIRIKA

REAL Madrid walipepeta Atletico Madrid 2-1 katika gozi la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na kuendeleza rekodi nzuri ya kushinda mechi zote sita za ufunguzi wa kipute hicho muhula huu wa 2022-23.

Rodrygo alifungulia Real ukurasa wa mabao kutokana na krosi ya Aurelien Tchouameni kunako dakika ya 18 kabla ya Vinicius Jr kufunga la pili baada ya kushirikiana na Federico Valverde katika dakika ya 36.

Mario Hermoso alirejesha Atletico mchezoni katika dakika ya 83 kabla ya kuonyeshwa kadi nyekundu dakika saba baadaye. Bao lake lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na Antoine Griezmann aliyewajibishwa na Atletico kwa mara ya kwanza msimu huu.

Hermoso alionyeshwa kadi ya kwanza ya manjano kwa kosa la kumsukuma Dani Carvajal kimakusudi kabla ya kumpiga kumbo Dani Ceballos mwishoni mwa kipindi cha pili wakati Griezmann alipokuwa akijiandaa kuchanja mpira wa kona.

Hata hivyo, ladha ya ushindi huo wa Real iliyeyushwa na nyimbo za mashabiki waliombagua Vinicius kwa msingi wa rangi huku baadhi wakimrushia vifaa mbalimbali uwanjani baada ya kufunga bao.

Chini ya kocha Carlo Ancelotti, Real kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 18, mbili kuliko nambari mbili Barcelona. Atletico wanakamata nafasi ya saba kwa pointi 10 sawa na Real Sociedad waliopepeta Espanyol 2-1.

Mara ya mwisho kwa Real kushinda mechi sita mfululizo za ufunguzi wa msimu wa La Liga ni 1987-88.

MATOKEO YA LA LIGA (Jumapili):

Atletico Madrid 1-2 Real Madrid

Osasuna 0-2 Getafe

Villarreal 1-1 Sevilla

Real Betis 2-1 Girona

Real Sociedad 2-1 Espanyol

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Arsenal wakomoa Brentford ugenini na kurejea kileleni mwa...

Limbukeni Monza waangusha miamba Juventus katika Ligi Kuu...

T L