• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Arsenal wakomoa West Ham United ugenini na kurejea nne-bora EPL

Arsenal wakomoa West Ham United ugenini na kurejea nne-bora EPL

Na MASHIRIKA

ARSENAL walipepeta West Ham United 2-1 uwanjani London Stadium mnamo Jumapili na kurejea katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Masogora hao wa kocha Mikel Arteta walishuka ugani wakiwa na ulazima wa kushinda baada ya washindani wao wakuu, Tottenham Hotspur kupiga Leicester City na kupaa hadi nafasi ya nne-bora kabla ya Arsenal kuwadengua.

Gabriel Magalhaes alifungia Arsenal bao la pili na la ushindi katika dakika ya 54 baada ya Rob Holding kufungua ukurasa wa mabao baada ya kushirikiana vilivyo na Bukayo Saka kunako dakika ya 38.

Awali, Jarrod Bowen alikuwa amerejesha West Ham mchezoni kwa kusawazisha mambo mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kujaza kimiani krosi ya Vladimir Coufal.

Arsenal kwa sasa wanajivunia alama 63, mbili zaidi kuliko Spurs wanaofunga nafasi ya tano. West Ham wanaofukuzia pia ubingwa wa Europa League, wanashikilia nafasi ya saba kwa pointi 52, tatu nyuma ya nambari sita Manchester United.

Tofauti na West Ham waliopigwa na Eintracht Frankfurt 2-1 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Europa League mnamo Aprili 28, Arsenal walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe uliowawezesha kupepeta Manchester United 3-1 ugani Emirates mnamo Aprili 23, 2022.

Licha ya kupiga hatua kubwa katika kipute cha Europa League, West Ham wamekuwa wakisuasua katika EPL huku wakipoteza sasa mechi tatu na kuambulia sare katika michuano minne iliyopita.

Ilivyo, matumaini ya West Ham kutinga nne-bora katika EPL yamedidimia na fursa nzuri zaidi kwao kufuzu kwa  soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao ni kunyanyua taji la Europa League, ikizingatiwa ushindani mkali kati ya Arsenal na Spurs ambao pia wanawania fursa ya kuingia ndani ya nne-bora katika EPL.

Arsenal wameshinda mechi saba kati ya tisa zilizopita ugenini na wanajivunia rekodi ya kupepeta West Ham West Ham mara 14 uwanjani London. Walitoka chini kwa mabao 3-0 na kulazimishia West Ham sare ya 3-3 ugenini mnamo 2020-21 kabla ya kusajili ushindi wa 2-0 katika mkondo wa kwanza wa EPL msimu huu mnamo Disemba 2021 uwanjani Emirates.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kiganjo Kings inalenga kupanda ngazi msimu huu

Polisi wakubaliwa kuvunja makazi ya Mchina

T L