• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Arsenal wapepea EPL

Arsenal wapepea EPL

Na MASHIRIKA

ARSENAL walifungua mwanya wa alama nane kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kukomoa Tottenham Hotspur 2-0 ugenini mnamo Jumapili.

Vijana hao wa kocha Mikel Arteta walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuchuma nafuu kutokana na kuteleza kwa mabingwa watetezi Manchester City waliotandikwa 2-1 na Manchester United mnamo uwanjani Old Trafford mnamo Jumamosi.

Kipa Hugo Lloris wa Spurs alibabatizwa na mpira kutoka kwa Bukayo Saka na akajifunga katika dakika ya 14 kabla ya nahodha Martin Odegaard kufungia Arsenal bao la pili dakika tisa kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa.

Ingawa Spurs walipata nafasi nyingi za kufunga katika kipindi cha pili, mafowadi wao walizidiwa ujanja na kipa mzoefu wa Arsenal, Aaron Ramsdale, aliyepangua na kudhibiti makombora ya Harry Kane, Ryan Sessegnon na Son Heung-min na mwishowe kutawazwa mchezaji bora wa mechi.

Ilikuwa mara ya tisa katika mashindano yote na mara saba katika EPL msimu huu kwa Spurs kujipata chini katika kipindi cha kwanza. Mechi dhidi ya Arsenal ilikuwa jukwaa maridhawa kwa Kane kufunga bao lake la 266 kambini mwa Spurs na kufikia rekodi ya nguli Jimmy Greaves.

Huku Arsenal wakijivunia sasa alama 47 kileleni mwa jedwali, matumaini ya Spurs kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora yalididimia. Kikosi hicho cha kocha Antonio Conte kwa sasa kinakamata nafasi ya tano kwa alama 33, tano nyuma ya nambari tatu Newcastle United ambao pia wametandaza jumla ya mechi 19.

Manchester United wanafunga mduara wa nne-bora kwa alama 38, moja nyuma ya Man-City ambao pia wametandaza mechi 18 sawa na Arsenal.

Ushindi kwa Arsenal katika pambano lao la 193 dhidi ya Spurs unatarajiwa sasa kuwapunguzia presha kadri wanavyosuka njama ya kuzamisha Man-United katika pambano lijalo la EPL ugani Emirates.

Spurs walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kulipiza kisasi baada ya kutandikwa 3-1 katika pambano la mkondo wa kwanza ligini msimu huu uwanjani Emirates.

Sawa na Spurs waliodengua Portsmouth 1-0 katika raundi ya tatu ya Kombe la FA, Arsenal pia walijitosa ulingoni wakiwa na motisha ya kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 3-0 dhidi ya Oxford United. Zawadi ya ushindi huo ni mtihani mgumu dhidi ya Manchester City katika raundi ya nne ya Kombe la FA huku Spurs wakipewa Preston North End.

Ushindi wa 4-0 dhidi ya Crystal Palace ndio matokeo ya kuridhisha zaidi ambayo Spurs wamesajili hivi karibuni huku wakipoteza sasa mechi nne kati ya tano zilizopita za EPL katika uwanja wao wa nyumbani. Ilikuwa mara yao ya kwanza kuondoka ugani bila kufunga Arsenal ligini tangu Novemba 2017.

Arsenal ambao hawajapoteza mechi yoyote kati ya 12 zilizopita ligini, wameshinda michuano sita kati ya saba katika EPL ugenini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Chelsea waangusha Palace ugani Stamford Bridge na...

Wazazi wa gredi ya 6 wapumua

T L