• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 2:08 PM
Arteta aahidi mashabiki wa Arsenal makuu

Arteta aahidi mashabiki wa Arsenal makuu

LONDON, Uingereza

KOCHA Mikel Arteta amewataka mashabiki wa Arsenal kutarajia makuu zaidi kwa imani kwamba ushindi wa 3-1 dhidi ya Chelsea mnamo Disemba 26 ni kiini cha ufufuo wa makali ya kikosi chake katika kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu.

Ushindi huo ulipunguza presha katika kambi ya Arsenal ambao waliwapa mashabiki wao ‘kitu’ cha kufurahia baada ya kukomesha rekodi mbovu iliyowashuhudia wakiokota alama mbili pekee kutokana na mechi saba za awali ligini.

Aidha, ilikuwa mara ya kwanza kwa Arsenal kushinda mchuano wa EPL tangu Novemba 1 walipowapokeza Manchester United kichapo cha 1-0 ugani Old Trafford.

Alexandre Lacazette alifungulia Arsenal ukurasa wa mabao kupitia penalti kabla ya Granit Xhaka na Bukayo Saka kufunga magoli mengine. Chelsea walifutiwa machozi na Tammy Abraham mwishoni mwa kipindi cha pili, dakika chache baada ya Jorginho Frello kupoteza penalti iliyopanguliwa na kipa Bernd Leno.

Hadi walipovaana na Chelsea katika mechi hiyo ya Disemba 26 ugani Emirates, Arsenal walikuwa wameshinda kikosi hicho cha kocha Frank Lampard mara mbili pekee kutokana na michuano 17 ya awali.

“Ni ushindi uliofanya siku kuwa spesheli. Ni tija na fahari tele kuangusha Chelsea kwa namna tulivyofanya. Haya ni matokeo ambayo ni kitulizo kikubwa kwa mashabiki wetu na ambayo yanastahili kuwa mwanzo wa kujiamini kwa kila mchezaji na ufufuo kwa kikosi kizima,” akasema Arteta.

Kwa upande wake, Lampard alikuwa mwingi wa lawama kwa wanasoka wake ambao walikosa fursa nzuri ya kupaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL.

“Nina hasira kwa sababu hii ni mechi tuliyopoteza kwa kutaka. Wachezaji walikuwa wazembe na utepetevu wao ukawapa wapinzani fursa ya kuwazidia maarifa katika kila idara. Uzembe ulitufanya kupoteza penalti muhimu na kutomakinikia frikiki iliyofungwa na Xhaka,” akasema Lampard.

Huku Arsenal wakiwa na alama 17 kutokana na mechi 15 za hadi kufikia sasa muhula huu, Chelsea wanajivunia pointi 25 sawa na Aston Villa waliowapepeta Crystal Palace 3-0 ugani Villa Park katika mojawapo ya mechi nyingine za Disemba 26.

Kikosi kilichotegemewa na Arteta dhidi ya Chelsea kilifanyiwa mabadiliko sita baada ya Arsenal kucharazwa 2-1 na Everton katika mechi ya awali. Arteta aliwapa chipukizi Saka, Gabriel Martinelli na Emile Smith Rowe fursa ya kudhihirisha uwezo wao uwanjani na ushirikiano wao ukazaa matunda.

Kwingineko, Manchester City walikaribia kilele cha jedwali baada ya kuwachabanga Newcastle United 2-0 ugani Etihad. Kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola sasa kinajivunia alama 26, tatu nyuma ya Everton waliorefusha mkia wa Sheffield United kwa kichapo cha 1-0 ugani Bramall Lane.

 

CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Masaibu ya Gor Mahia kwenye CAF Champions League

Linturi alaumu Rais kwa kupuuza kilio cha Wakenya