• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 10:18 AM
Masaibu ya Gor Mahia kwenye CAF Champions League

Masaibu ya Gor Mahia kwenye CAF Champions League

Na CHRIS ADUNGO

MATUMAINI finyu ya Gor Mahia kusonga mbele katika kampeni za Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) msimu huu yalizimwa na CR Belouizdad ya Algeria mnamo Disemba 26 baada ya miamba hao wa soka ya humu nchini kupondwa 6-0 jijini Algiers.

Mikakati duni na maandalizi mabovu yamehusishwa na matokeo hayo mabaya ya Gor Mahia ambao walitua Algiers siku moja kabla ya mechi. Kikosi hicho kilichokabiliwa na panda-shuka tele za usafiri kililazimika kupitia jijini Doha, Qatar kabla ya kuelekea Algiers.

Kabla ya kuondoka humu nchini kwa minajili ya mechi hiyo iliyopangiwa awali kusakatwa Disemba 23 kabla ya Gor Mahia kuomba Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) iratibu upya, wanasoka wa K’Ogalo walikuwa wamesusia mazoezi wakilalamikia kutolipwa malimbikizi ya mishahara na marupurupu.

“Ni matokeo ya aibu kusajiliwa na kikosi kikubwa kufu ya Gor Mahia. CAF ni kivumbi chenye ushindani mkali na washiriki huhitaji maandalizi ya kutosha kwa wakati ufaao,” akasema shabiki kupitia mtandao wake kijamii.

“Ni fedheha kubwa kwa usimamizi wa kikosi kutuma wanasoka kucheza kwa ajili ya kucheza tu bila ya maslahi yao kushughulikiwa,” akasema shabiki mwingine katika kauli iliyoshadidiwa na mchezaji mmoja mzoefu wa Gor Mahia aliyetaka jina lake libanwe aliyesema:

“Hakuna yeyote aliyeshiriki mazoezi wala kujifua kikamilifu kwa ajili ya mchuano huo. Hatukuwa tayari kwa mechi dhidi ya Belouizdad na hakuna jinsi ambavyo matokeo bora yangepatikana katika hali kama hiyo. Tunawaomba radhi mashabiki wetu.”

Gor Mahia walifuzu kuvaana na Belouizdad baada ya kubandua APR ya Rwanda kwa mabao 4-3 kwenye raundi ya kwanza ya mchujo. Wanatarajiwa sasa kurejea humu nchini mnamo Disemba 28 kuanza kujifua kwa gozi la marudiano litakalochezewa ugani Nyayo, Nairobi mnamo Januari 5, 2021.

Kiungo Amir Sayoud, 30, alifungia Belouizdad mabao matatu kabla ya mengine kufumwa wavuni na Hamza Bellahouel, Larbi Tabti na Maecky Ngombo katika mechi hiyo iliyochezewa ugani 1955 Stadium.

Matokeo hayo yanamaanisha kwamba Gor Mahia wanaotiwa makali na kocha Sammy ‘Pamzo’ Omollo wa Posta Rangers, watakuwa na ulazima wa kusajili ushindi wa angalau 7-0 katika mchuano wa mkondo wa pili ili kufuzu kwa hatua ya makundi ya CAF Champions League kwa mara ya kwanza katika historia.

Iwapo watabanduliwa kwenye CAF Champions League, jambo ambalo ni dhahiri, Gor Mahia watashuka hadi kipute cha Kombe la Mashirikisho (CAF Confederation Cup) kwa mara nyingine.

Matumaini yao ya kusonga mbele kwenye Confederation Cup mwaka jana yalizimwa na USM Alger ya Algeria iliyowabandua kwa jumla ya mabao 6-1 baada ya kichapo cha 4-1 ugenini na 2-0 ugani MISC Kasarani kwenye mchuano wa mkondo wa pili mnamo Septemba 2019.

Gor Mahia walirejea kushiriki soka ya Champions League mnamo Februari 2017 ambapo walipangwa kuvaana na Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea katika raundi ya kwanza ya mchujo. Waliambulia sare ya 1-1 ugenini kabla ya kusajili ushindi wa 2-0 nyumbani.

Ufanisi huo uliwapa tiketi ya kuchuana na Esperance ya Tunisia mnamo Machi 2018 ambapo walibanduliwa kwa bao 1-0 baada ya kuambulia sare tasa katika mkondo wa kwanza jijini Nairobi.

Kichapo hicho kiliwafanya kushushwa ngazi kushiriki michuano ya Kombe la Mashirikisho ambapo walipangwa kukutana na SuperSport United ya Afrika Kusini kwenye mchujo.

Walifuzu kwa hatua ya makundi kwa kanuni ya wingi wa mabao ya ugenini (2-2) baada ya kusajili ushindi wa 1-0 nyumbani kabla ya chombo chao kuzamishwa kwa kichapo cha 2-1 ugenini katika uwanja wa Lucas Moripe.

Walitiwa baadaye katika Kundi D kwa pamoja na Yanga SC ya Tanzania, USM Alger ya Algeria na Rayon Sports ya Rwanda. Waliambulia sare ya 1-1 dhidi ya Rayon Sports, wakapoteza 2-1 dhidi ya USM Alger kabla ya kupepeta Yanga 3-2.

Hata hivyo, kichapo cha 2-1 dhidi ya Rayon kilizamisha matumaini ya miamba hao wa Kenya kusonga mbele kwa hatua ya robo-fainali. Hii ni baada ya Rayon kujizolea alama moja muhimu dhidi ya USM Alger ugenini na kusonga mbele kutoka Kundi D.

Safari ya Gor Mahia kwenye Champions League mnamo 2018 ilianza kwa ushindi dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi. Katika mkondo wa kwanza, walisajili ushindi wa 1-0 uwanjani Kasarani kabla ya Big Bullets kusajili matokeo sawa na hayo wakati wa marudiano. Mshindi wa mechi hiyo aliamuliwa kupitia mikwaju ya penalti ambapo kipa Boniface Oluoch alipangua makombora mawili na kusaidia Gor Mahia kuibuka na ushindi wa 4-3.

Matumaini ya Gor Mahia kusonga mbele kwenye Champions League mnamo Disemba 2018 yalizimwa ghafla na Lobi Stars ya Nigeria waliowapiga 2-0 kwenye mchuano wa raundi ya pili ya mchujo.

Austin Ogunye na Alimi Sikiru walifungia Lobi Stars katika mechi ya marudiano baada ya Gor Mahia kusajili ushindi wa 3-1 nyumbani wakati wa mechi ya mkondo wa kwanza.

Kwa mara nyingine, Gor Mahia walishuka ngazi hadi mechi za Confederation Cup na wakapangwa pamoja na New Star de Doula ya Cameroon kwenye mchujo.

Baada ya kushinda 2-1 nyumbani, walilazimisha sare tasa jijini Doula na wakafuzu kwa hatua ya makundi. Katika Kundi D, walipigwa 2-1 ugenini na Petro Atletico ya Angola, 1-0 na NA Hussein Dey ya Algeria na 4-0 dhidi ya SC Zamalek ya Misri.

Hata hivyo, walifaulu kufuzu kwa robo-fainali baada ya kupepeta Zamalek 4-2, Hussein Dey 2-0 na Petro Atletico 1-0 nyumbani. Licha ya kusonga mbele, Gor Mahia walipokezwa kichapo cha mabao 5-1 ugenini na Renaissance Sportive de Berkane ya Morocco wlaiowacharaza 2-0 nyumbani.

Mnamo 2019-20, Gor Mahia waliwapepeta Aigle Noir ya Burundi 5-1 nyumbani baada ya kuambulia sare tasa ugenini jijini Bujumbura.

You can share this post!

Kura ya Matungu kipimo cha umaarufu wa Mudavadi

Arteta aahidi mashabiki wa Arsenal makuu