• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Manchester United wapiga Manchester City breki kali ligini

Manchester United wapiga Manchester City breki kali ligini

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walikomesha mbio zilizoshuhudia Manchester City wakisajili ushindi katika msururu wa mechi 21 katika mashindano yote ya msimu huu kwa kuwapokeza kichapo cha 2-0 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Etihad mnamo Jumapili.

Licha ya kichapo, Man-City ya kocha Pep Guardiola wangali wanajivunia pengo la alama 11 kileleni mwa jedwali. Masogora wa Guardiola kwa sasa wanajivunia alama 65 kutokana na mechi 28 zilizopita.

Alama tatu zilizotiwa kapuni na Man-United ziliwarejesha katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali na kwa sasa wana pointi 54, saba kuliko Chelsea wanaofunga orodha ya nne-bora. Leicester City ya kocha Brendan Rodgers wanakamata nafasi ya tatu kwa alama 53.

Man-United ambao kwa sasa wametandaza jumla ya mechi 22 za EPL ugenini bila ya kushindwa, walifungua karamu ya mabao katika dakika ya pili kupitia penalti ya Bruno Fernandes. Mkwaju huo ulikuwa zao la fowadi Anthony Martial kuchezewa visivyo na Gabriel Jesus ndani ya kijisanduku cha Man-City.

Rodri Hernandez nusura asawazishie Man-City mwishoni mwa kipindi cha kwanza ila kombora lake likabusu mwamba wa goli la Man-United waliopata bao la pili kupitia Luke Shaw aliyekamilisha krosi ya Marcus Rashford katika dakika ya 50.

Kichapo ambacho Man-City walipokezwa kilikuwa cha kwanza tangu wapigwe 2-0 na Tottenham Hotspur mnamo Novemba 21, 2020.

Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo wakiwa na kiu ya kujinyanyua baada ya kutofunga bao katika jumla ya michuano mitatu ya awali.

Baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya Real Sociedad kwenye marudiano ya hatua ya 32-bora kwenye Europa League mnamo Februari 25, 2021, Man-United walikabwa koo kwa sare tasa nyinginezo ligini dhidi ya Chelsea na Crystal Palace mtawalia.

Ushindi dhidi ya Man-City sasa unaweka kikosi hicho cha Solskjaer katika nafasi nzuri zaidi ya kumaliza kampeni za msimu ndani ya mduara wa nne-bora na kufuzu kwa soka ya UEFA licha ya ushindani mkali kutoka kwa Leicester, Chelsea, Everton, West Ham United, Tottenham na Liverpool ambao ni mabingwa watetezi.

Man-United waliwashinda Man-City katika michuano yote miwili ya EPL msimu uliopita wa 2019-20. Solskjaer kwa sasa ndiye kocha wa kwanza wa Man-united kuwahi kuongoza masogora wake kushinda mechi tatu mfululizo dhidi ya Man-City ugenini tangu Novemba 1993 na Novemba 2000.

Isitoshe, ndiye kocha wa kwanza wa katika historia ya Man-United kuwahi kushinda michuano yake mitatu ya kwanza ugenini dhidi ya Man-City katika mashindano yote.

Man-City walipigwa kwa mara ya kwanza tangu Novemba 2020 walipozabwa na Tottenham 2-0. Kichapo cha Jumapili usiku kilikomesha rekodi ya kutoshindwa kwao katika jumla ya mechi 28 katika mashindano yote ya msimu huu.

Man-City kwa sasa wanajiandaa kuvanaa na Southampton katika mechi ya EPL itakayowakutanisha ugani Etihad mnamo Machi 10 kabla ya kuwaendea Fulham uwanjani Craven Cottage siku tatu baadaye.

Kwa upande wao, Man-United wamepangiwa kuvaana na AC Milan ya Italia kwenye mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya Europa League mnamo Machi 11 kabla ya kualika West Ham United ya kocha David Moyes ligini mnamo Machi 14, 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali isubire ripoti kuhusu AstraZeneca

Bale na Kane waongoza Tottenham kuwateremkia Crystal Palace...