• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Barcelona wakomoa Rayo Vallecano na kutinga robo-fainali za Copa del Rey

Barcelona wakomoa Rayo Vallecano na kutinga robo-fainali za Copa del Rey

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alirejea uwanjani baada ya kutumikia marufuku ya mechi mbili na kusaidia Barcelona kutoka nyuma na kuwapepeta Rayo Vallecano 2-1 katika ushindi uliowapa tiketi ya robo-fainali za Copa del Rey msimu huu.

Rayo ambao wanashikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la Ligi ya Daraja la Pili nchini Uhispania, walitwaa uongozi kupitia bao la Fran Garcia Torres kunako dakika ya 63.

Hata hivyo, Barcelona walisawazisha dakika sita baadaye kupitia kwa Messi aliyekuwa akinogesha mchuano wa kwanza tangu apigwe marufuku ya mechi mbili tangu aonyeshwe kadi nyekundu kwa mara ya kwanza akiwa mchezaji wa Barcelona mnamo Januari 17.

Messi alipokezwa adhabu hiyo kwa kumkabili visivyo kiungo Asier Villalibre katika fainali ya Spanish Super Cup iliyoshuhudia Athletic Bilbao wakisajili ushindi wa 3-2 jijini Seville.

Bao la Messi dhidi ya Rayo mnamo Januari 27 lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na fowadi Antoine Griezmann ambaye ni raia wa Ufaransa.

Bao la ushindi kwa upande wa Barcelona lilijazwa kimiani na kiungo mkabaji Frenkie de Jong dakika 10 kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Goli hilo la De Jong lilichangiwa na Messi ambaye kwa pamoja na Jordi Alba, walitatiza sana mabeki wa Rayo.

Barcelona wanajivunia rekodi ya kutia kibindoni taji la Copa del Rey mara 30 na kampeni za msimu huu katika kipute hicho zinampa kocha Ronald Koeman matumaini ya kutwaa kombe katika msimu wake wa kwanza wa ukufunzi uwanjani Camp Nou.

Kufikia sasa, ni pengo la alama 10 ndilo linatamalaki kati ya Barcelona na Atletico Madrid kileleni mwa jedwali la La Liga na miamba hao wa soka ya Uhispania wamepangwa kukutana na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa kwenye hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Atletico na Real Madrid walibanduliwa mapema kwenye kampeni za Copa del Rey msimu huu na tukio hilo linafanya Barcelona kupigiwa upatu wa kutwaa taji hilo muhula huu.

Hata hivyo, washindani wakuu wa Barcelona wanatarajiwa kuwa Sevilla waliotinga robo-fainali za Copa del Rey mnamo Januari 27 baada ya kuwapepeta Valencia 3-0.

Real Betis, Villarreal na Levante ni vikosi vingine ambavyo tayari vimefuzu kwa hatua ya nane-bora ya kivumbi cha Copa del Rey msimu huu baada ya kusajili ushindi kwenye michuano yao ya Januari 26, 2021.

You can share this post!

Zaidi ya hospitali 17 za umma kuzinduliwa Nairobi

Wafalme wa kudandia madaraka