• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:50 AM
Barcelona yampa Lionel Messi likizo ya mapema kujiandaa kwa fainali za Copa America

Barcelona yampa Lionel Messi likizo ya mapema kujiandaa kwa fainali za Copa America

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi atakosa mchuano wa mwisho wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) msimu huu utakaowakutanisha waajiri wake Barcelona na Eibar katika uwanja wa Manispaa ya Ipurua.

Kwa mujibu wa kocha Ronald Koeman, Messi amepewa likizo itakayompa nafasi maridhawa ya kupumzika kabla ya kipute cha Copa America kung’oa nanga.

Nyota huyo raia wa Argentina alipewa idhini ya kukosa pia kipindi cha mazoezi kilichoandaliwa na Barcelona mnamo Ijumaa.

Chini ya Koeman, Barcelona tayari wameondolewa kwenye mbio za kuwania ubingwa wa La Liga muhula huu na kwa sasa wana uhakika wa kumaliza kampeni za kipute hicho nje ya mduara wa mbili-bora kwa mara ya kwanza tangu 2007-08.

“Messi ana idhini ya kuanza mapema likizo yake kadri anavyojiandaa kwa Copa America. Anastahili kupumzika sasa ikizingatiwa kwamba ni miongoni mwa wachezaji ambao wamewajibishwa katika takriban kila mchuano msimu huu,” ikasema sehemu ya taarifa ya Barcelona.

Messi, 33, tayari amewajibishwa na Barcelona katika jumla ya michuano 47 msimu huu wa 2020-21 na amefungia kikosi hicho mabao 38.

Sogora huyo anahusishwa pakubwa na uwezekano wa kuyoyomea Uingereza kuungana na kocha wake wa zamani, Pep Guardiola kambini mwa Manchester City au kutua Ufaransa kuchezea Paris Saint-Germain (PSG) wanaojivunia huduma za nyota wa zamani wa Barcelona, Neymar Jr.

Kichapo cha 2-1 ambacho Barcelona walipokezwa na Celta Vigo mnamo Mei 16 kiliwaondoa Barcelona kwenye kinyang’anyiro cha kufukuzia taji la La Liga ambacho sasa kinawaniwa na Atletico Madrid na Real Madrid.

Fainali za Copa America ziliahirishwa kutoka mwaka wa 2020 kwa sababu ya janga la corona na sasa zimeratibiwa kupigwa kati ya Juni 13 na Julai 10 nchini Argentina.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Barabara hatari eneo la Ngunguru-Karatina

Chelsea kutumia Abraham na Kepa kushawishi Spurs kuwapa...