• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Barcelona yazamisha Atletico na kufungua pengo la alama tatu kileleni mwa jedwali la La Liga

Barcelona yazamisha Atletico na kufungua pengo la alama tatu kileleni mwa jedwali la La Liga

Na MASHIRIKA

BARCELONA walifungua mwanya wa alama tatu kati yao na mabingwa watetezi Real Madrid kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) baada ya kucharaza Atletico Madrid 1-0 mnamo Jumapili ugani Wanda Metropolitano.

Ousmane Dembele ndiye alifunga bao la pekee katika mchuano huo baada ya kukamilisha krosi ya Pablo Gavi kunako dakika ya 22.

Atletico walipoteza nafasi murua ya kusawazisha mwishoni mwa kipindi cha pili kupitia kwa Antoine Griezmann aliyeshuhudia kombora lake likiondolewa na Ronald Araujo kwenye mstari wa goli.

Pande zote mbili zilikamilisha mechi hiyo na wachezaji 10 uwanjani baada ya Stefan Savic wa Atletico na Ferran Torres kuonyeshwa kadi nyekundu kwa utovu wa nidhamu mwishoni mwa kipindi cha pili.

Barcelona, ambao wamepoteza mechi moja pekee ligini msimu huu, sasa wanaselelea kileleni kwa alama 41 kutokana na michuano 16. Walichuma nafuu kutokana na kujikwaa kwa Real waliopigwa 2-1 na Villarreal mnamo Jumamosi.

Diego Simeone alikuwa akisimamia mechi yake ya 418 ya La Liga kambini mwa Atletico na sasa ndiye anayeshikilia rekodi ya kuwahi kusimamia michuano mingi zaidi akidhibiti mikoba ya kikosi kimoja cha La Liga.

Pambano dhidi ya Barcelona lilikuwa la tano kwa Atletico kupoteza kutokana na mechi 16 za La Liga muhula huu. Klabu hiyo sasa inakamata nafasi ya tano jedwalini kwa alama 27, moja nyuma ya nambari nne Real Betis waliokomoa Rayo Vallecano 2-1. Real Sociedad walichapa Almeria 2-0 nao Sevilla wakakung’uta Getafe 2-1.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

AC Milan na AS Roma nguvu sawa katika Serie A huku Napoli...

Man-City wadengua Chelsea katika raundi ya tatu ya Kombe la...

T L