• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Beki Kalidou Koulibaly abanduka Chelsea na kuyoyomea Saudi Arabia kuchezea Al-Hilal

Beki Kalidou Koulibaly abanduka Chelsea na kuyoyomea Saudi Arabia kuchezea Al-Hilal

Na MASHIRIKA

KALIDOU Koulibaly, 32, amekuwa mchezaji wa hivi punde zaidi wa Chelsea kuyoyomea Saudi Arabia baada ya kusajiliwa na Al-Hilal kwa kima cha Sh3.6 bilioni.

Beki huyo kisiki raia wa Senegal anajiunga na kipute cha Saudi Pro League siku chache baada kiungo mzoefu Ruben Neves kubanduka Wolverhampton Wanderers na kutua kambini mwa Al-Hilal kwa Sh8.4 bilioni.

Kiungo matata wa Chelsea, N’Golo Kante, tayari ameingia katika sajili rasmi ya mabingwa wa Saudia, Al-Ittihad, huku kipa Edouard Mendy akiwa pua na mdomo kutwaliwa na Al-Ahli.

Mjerumani Kai Havertz naye anatazamiwa kuondoka ugani Stamford Bridge na kujiunga na Arsenal kwa Sh11.6 bilioni, siku chache baada ya kiungo raia wa Croatia, Mateo Kovacic, kusajiliwa na Manchester City kwa Sh5.3 bilioni.

Chelsea wanazidi kujisuka upya chini ya mkufunzi Mauricio Pochettino ambaye tayari amesajili wavamizi Christopher Nkunku, Nicolas Jackson na Dujuan Richards kutoka RB Leipzig (Ujerumani), Villarreal (Uhispania) na Phoenix All Stars Academy (Jamaica) mtawalia.

Koulibaly alisajiliwa na Chelsea kwa mkataba wa miaka minne mnamo Julai mwaka jana baada ya kuagana na Napoli ya Italia. Alitua ugani Stamford Bridge akijivunia tajriba pevu katika soka ya kimataifa na bara Ulaya baada ya kusaidia Senegal kutwaa Kombe la Afrika (AFCON) 2022 na kuongoza Napoli kujizolea Italian Cup 2020.

Hata hivyo, alichezea Chelsea mara 32 katika mashindano yote huku akifunga mabao mawili pekee kutokana na mechi 23 za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

“Kuanzia mchuano wa kwanza hadi wa mwisho, ilikuwa tija na fahari kuvalia jezi za Chelsea. Japo msimu jana haukuwa ule tuliotarajia, nashukuru mashabiki na kila mmoja aliyenifanya kufurahia maisha Stamford Bridge,” akasema beki huyo kupitia Twitter.

Koulibaly anaendeleza mtindo wa hivi karibuni ambao umeshuhudia masogora wa haiba kubwa wakiondoka bara Ulaya na kuyoyomea Saudi Arabia tangu supastaa Cristiano Ronaldo abanduke Manchester United na kujiunga na Al-Nassr mnamo Januari 2023.

Karim Benzema naye alijiunga na Al-Ittihad baada ya kuagana na Real Madrid mwishoni mwa msimu huu huku Thomas Partey (Arsenal), Bernardo Silva (Man-City) na Hakim Ziyech (Chelsea) wakihusishwa pia na uwezekano mkubwa wa kuyoyomea Saudia.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Polisi wanasa washukiwa 17 na misokoto 500 ya bangi katika...

Mzozo wa UDA katika kaunti ya Rais

T L