• Nairobi
  • Last Updated December 9th, 2023 5:55 AM
Bingwa Chebet abeba tuzo ya Mchezaji Bora

Bingwa Chebet abeba tuzo ya Mchezaji Bora

NA GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Boston Marathon Evans Chebet analenga kutawala New York Marathon mnamo Novemba 6, 2022.

Chebet, 33, alifichua hayo jijini Nairobi jana baada ya kutawazwa mshindi wa tuzo ya kifahari ya Mwanamichezo Bora wa Aprili, ya LG/SJAK.

Wenyeji wa tuzo hiyo Chama cha Waandishi wa Michezo Kenya (SJAK), pamoja na wadhamini kampuni ya kielektroniki ya LG, walimpa Chebet mashine ya kufua nguo ya thamani ya Sh90,000 pamoja na tuzo.

Chebet alifurahia zawadi hiyo akisema ni motisha tosha ya kusaka mafanikio zaidi.

“Nashukuru sana. Nitajitahidi zaidi ili nishinde tena. Nilipopigiwa simu kuwa mimi ni mshindi, sikuamini. Ni motisha kubwa sana,” alisema mwanariadha huyo anayefanyia mazoezi mjini Kapsabet, Kaunti ya Nandi.

Ushindi wa Boston Marathon ni wake wa kwanza kabisa katika Ligi ya Marathon Kuu Duniani (WMM) inayojumuisha zile za Tokyo, Boston, London, Berlin, Chicago na New York.

Alimaliza Berlin Marathon 2016 katika nafasi ya tatu, London Marathon 2021 nambari nne na kukosa kukamilisha Boston Marathon ya 2018.

Katika makala ya mwaka huu ya Boston Marathon, Chebet aliduwaza mabingwa wa zamani Lawrence Cherono, Lemi Birhanu na Yuki Kawauchi; Benson Kipruto aliyekuwa akitetea taji hilo; na mfalme wa New York Marathon 2019, Geoffrey Kamworor, miongoni mwa majina mengine makubwa.

Katika kuibuka mshindi wa tuzo hiyo ya LG/SJAK, Chebet alilemea mabingwa Peres Jepchirchir (Boston Marathon), Judith Cheptum (Paris Marathon) na Maurine Chepkemoi (Enschede Marathon).Pia bingwa wa duru ya Afrika ya Mbio za Magari ya Equator Rally Karan Patel.

Isitoshe alipiku mabondia Teresia Wanjiru (Light welter), Everlyne Akinyi (Welter), Elizabeth Andiego (Light heavy), David Karanja (Fly) na Shaffi Bakari (Bantam) waliozoa dhahabu kwenye mashindano ya Afrika Zoni 3 nchini Congo hivi majuzi.

Mkurugenzi Mkuu wa LG Electronics kanda ya Afrika Mashariki, Sa Nyoung Kim, alisema wataendelea kusaidia SJAK kuwapa motisha wanamichezo wa fani mbalimbali kupitia tuzo hiyo.

Rais wa SJAK, Chris Mbaisi, alishukuru LG kuendelea kudhamini tuzo hata wakati huu mgumu wa kiuchumi.

  • Tags

You can share this post!

Wanasiasa wasukumwa kueleza mipango ya kuinua utalii

Waruguru aponda wawaniaji UDA

T L