• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Brigid Kosgei sasa kuwa balozi wa kutangaza Stanbic Bank

Brigid Kosgei sasa kuwa balozi wa kutangaza Stanbic Bank

Na GEOFFREY ANENE

Mshikilizi wa rekodi ya mbio za kilomita 42 ya wanawake Brigid Kosgei amepata zawadi ya mapema kabla ya kusherehekea kugonga umri wa miaka 27 hapo Februari 20 baada ya kutajwa kuwa balozi wa benki ya Stanbic Bank Kenya.

Katika mkataba wake na benki hiyo wa miaka miwili, ambao pande hizo zilisaini Februari 4 jijini Nairobi, malkia huyo wa mataji mawili ya mbio za kifahari za London Marathon na Chicago Marathon atakuwa sura ya bidhaa ya benki hiyo ya ‘It Can Be’. Mradi huo unalenga kuwapa nguvu wanawake na mashirika madogomadogo ya kibiashara.

Milionea huyo alishukuru benki ya Stanbic akisema ni heshima kubwa kufanywa kuwa balozi wake na kuapa kutumia fursa hiyo kuhamasisha umuhimu wa masomo na michezo kwa mtoto wa kike.

“Sikukamilisha masomo kwa sababu wazazi wangu hawakujiweza kifedha kunilipia karo na kwa hivyo najitahidi kupatia watoto wangu elimu nzuri pamoja na kuwasukuma katika michezo. Inafurahisha kuwa Stanbic Bank inataka kuinua wanawake katika nyanja hizo,” alisema Kosgei ambaye ni mmoja wa wakimbiaji watakaowakilisha Kenya katika mbio za kilomita 42 kwenye Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan mwezi Julai/Agosti mwaka huu.

Aidha, mtimkaji huyo, ambaye aliweka rekodi ya dunia ya saa 2:14:04 akihifadhi ubingwa wake wa Chicago Marathon mwaka 2019, alisalia mwingi wa matumaini kuwa rekodi hiyo inaweza kuimarishwa zaidi kupitia kubadilisha mazoezi yake. “Siwezi kubashiri ni lini rekodi hiyo yangu itafutwa, hasa kwa sababu janga la corona limeleta changamoto nyingi.

Hata hivyo, mazungumzo yote ya rekodi mpya hayafai kuwa kwangu tu kwa sababu kuna wakimbiaji wengine wakali kama mabingwa wa dunia Ruth Chepng’etich (marathon) na Peres Jepchirchir (nusu-marathon),” alisema Kosgei ambaye analenga kutimka mbio za mita 5,000 uwanjani ili kuimarisha kasi yake.

You can share this post!

Museveni akabidhiwa nakala za kesi ya Bobi Wine kutaka...

Lugha kama chombo cha mawasiliano baina ya binadamu