• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Chelsea wakomoa Leicester City na kupepea kileleni mwa jedwali la EPL

Chelsea wakomoa Leicester City na kupepea kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

VIONGOZI wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Chelsea, waliendeleza ubabe wao katika kipute hicho muhula huu kwa kupepeta Leicester City 3-0 uwanjani King Power.

Ushindi huo ulidumisha Chelsea kileleni mwa jedwali kwa alama 29, sita zaidi kuliko Manchester City ambao ni mabingwa watetezi.

Chini ya kocha Thomas Tuchel, Chelsea walifuma wavuni mabao mawili katika kipindi cha kwanza kupitia Antonio Rudiger na N’Golo Kante kabla ya Christian Pulisic kufunga ukurasa wao wa magoli katika dakika ya 71.

Chelsea waliopoteza nafasi nyingi za wazi, walishuhudia mabao yao matatu yakikosa kuhesabiwa na refa baada ya kubainika kwamba Hudson-Odoi, Reece James na Pulisic walicheka na nyavu za wenyeji wao wakiwa wameotea.

Mbali na kufungwa mabao manne pekee kutokana na mechi 12 zilizopita, kikubwa kinachoaminisha mashabiki wa Chelsea ni matokeo bora ya kikosi chao hata wakati huu wanapokosa huduma za wavamizi matata Romelu Lukaku na Timo Werner wanaouguza majeraha.

Hakuna kikosi kingine cha EPL kinachojivunia idadi kubwa zaidi ya wachezaji tofauti ambao wametikisa nyavu za wapinzani kufikia sasa muhula huu kuliko Chelsea ambayo imetoa wafungaji 15.

Huku ushindi wa Chelsea ukiendeleza masaibu ya Leicester ligini, kocha Brendan Rodgers sasa anakabiliwa na presha tele ya kupigwa kalamu ugani King Power. Leicester sasa wanajivunia alama 15 sawa na Everton watakaovaana leo na Man-City uwanjani Etihad.

Chini ya Rodgers anayehusishwa pakubwa na mikoba ya Manchester United iwapo Ole Gunnar Solskjaer atatimuliwa ugani Old Trafford, Leicester wameshinda mechi nne, kuambulia sare mara tatu na kupoteza michuano mitano kati ya 12 iliyopita ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

TAHARIRI: Tushabihiane na hadhi yetu katika riadha

Afueni kwa wakimbizi

T L