• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 5:50 PM
Chepngetich aingia Chicago Marathon kutetea taji

Chepngetich aingia Chicago Marathon kutetea taji

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Ruth Chepngetich atatetea taji lake la Chicago Marathon nchini Amerika mnamo Oktoba 8, 2023.

Ametoa ithibati ya kushiriki, huku baadhi ya wapinzani wake wakuu wakiwa ni bingwa wa London Marathon Sifan Hassan kutoka Uholanzi na mshikilizi wa rekodi ya kitaifa ya Amerika ya marathon Emily Sisson.

Chepngetich aliibuka malkia wa Chicago Marathon 2022 kwa saa 2:14:18, akikosa rekodi ya dunia ya Mkenya Brigid Kosgei ya 2:14:04 kwa sekunde 14 pekee. Huenda atavizia rekodi hiyo ya Kosgei tena.

Sifan atakayekuwa akishiriki marathon yake ya pili anatarajiwa kutoa ushindani mkali baada ya kupata motisha ya kutawala London Marathon katika jaribio lake la kwanza mwezi Aprili.

Chepngetich atajaribu kutwaa taji la Chicago Marathon kwa mara ya tatu mfululizo. “Napanga kutetea taji langu na kuimarisha muda wangu. Hakuna mbio zinazonichangamsha duniani kama Chicago Marathon,” alisema Chepngetich.

Jijini London mwezi Aprili, Sifan alisimama mara mbili mapema katika mbio hizo za kilomita 42, lakini akaziba mwanya wa karibu nusu dakika kati yake na wakimbiaji waliokuwa mbele akishinda taji kwa rekodi ya kitaifa ya Uholanzi ya 2:18:33.

Analenga kushiriki Riadha za Dunia uwanjani jijini Budapest, Hungary kabla ya kujitosa katika Chicago Marathon.

Sisson anashikilia rekodi ya Amerika ya 2:18:29. Chicago Marathon 2023 inatarajiwa kuvutia washiriki 45, 000.

  • Tags

You can share this post!

IPOA yachunguza kisa cha kijana kuuawa kwa kupigwa risasi...

Sacco ya wajane yazinduliwa Kwale

T L