• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 6:55 AM
Cheruiyot tayari kuonyesha bingwa wa Olimpiki Ingebrigtsen kivumbi Diamond League

Cheruiyot tayari kuonyesha bingwa wa Olimpiki Ingebrigtsen kivumbi Diamond League

Na AYUMBA AYODI

MSHINDI wa medali ya fedha ya Olimpiki ya mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot yuko tayari kujinyanyua anapojiandaa kutetea taji lake la Riadha za Diamond League jijini Zurich nchini Uswisi mnamo Alhamisi.

Cheruiyiot, ambaye anajivunia mataji ya Diamond League ya mwaka 2017, 2018 na 2019, atakuwa akitimka kwa mara ya kwanza tangu Olimpiki za Tokyo 2020 alipopoteza dhidi ya Jakob Ingebrigtsen kutoka Norway katika fainali.

“Niko tayari kwa fainali ambayo pengine itakuwa mbio yangu ya mwisho msimu huu,” alisema bingwa huyo wa dunia wa mwaka 2019.

Ili kufuzu kushiriki fainali jijini Zurich, Cheruiyot alitawala duru za Doha (dakika 3:30.48), Stockholm (3:32.30) na Monaco (3:28.28) mtawalia.

“Lengo langu mwaka 2022 ni kutetea taji la dunia na pia kushiriki michezo ya Jumuiya ya Madola,” alisema Cheruiyot akiwa katika msafara wa timu ya Wakenya iliyosafiri nchini Uswisi siku ya Jumatatu.

Wakenya Abel Kipsang, Ronald Kwemoi na Charles Simotwo pia watashiriki mbio za mita 1,500.

Macho yatakuwa kwa bingwa wa Olimpiki mita 1,500 Faith Chepng’etich katika kitengo cha kinadada atakayefufua uhasama dhidi ya Mholanzi Sifan Hassan.

Bingwa wa Olimpiki mbio za mita 800 Emmanuel Koir na mshindi wa nishani ya fedha Ferguson Rotich watakuwa mawindoni kupiga breki Marco Arop kutoka Canada aliyewaduwaza katika duru ya Prefontaine Classic mnamo Agosti 21 na Lausane mnamo Agosti 26 mtawalia.

Fainali ya Diamond League itafanyiwa katika eneo moja kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 2021. Washindi wa vitengo vyote 32 watafahamika siku hiyo.

You can share this post!

KINA CHA FIKIRA: Wakati ni sasa, tumia leo kutengeneza...

TAHARIRI: Kikosi maalumu kitumwe Laikipia