• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Coe afurahia juhudi za Kenya kuimarisha vita dhidi ya pufya

Coe afurahia juhudi za Kenya kuimarisha vita dhidi ya pufya

AYUMBA AYODI Na GEOFFREY ANENE

RAIS wa Shirikisho la Riadha Duniani Sebastian Coe amefurahia hatua ya Kenya kuahidi kuwekeza raslimali zaidi katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Katika taarifa kwa Waziri wa Michezo, Ababu Namwamba mnamo Jumamosi, Coe alipongeza mpango wa serikali wa kukabiliana na hatari ya kufanya uovu huo.

Taarifa ya Coe inapatia Kenya matumaini ya kuepuka adhabu ya kupigwa marufuku. Hata hivyo, hatma ya Kenya itajulikana wakati wa mkutano wa shirikisho hilo pamoja na Kitengo cha Riadha cha Maadili (AIU) na Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya duniani (WADA) mjini Monte Carlo, Monaco hapo Jumanne.

Ingawa mkutano huo ni wa kuangalia upya hali ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli kote duniani, Kenya inatarajiwa kuzungumziwa sana kutokana na ongezeko la visa vya uhalifu huo miongoni mwa wanariadha wake.

Zaidi ya wanariadha 20 kutoka Kenya wameadhibiwa na AIU na Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli nchini (ADAK) kwa makosa mbali mbali tangu Januari 2022.

“Napongeza serikali ya Kenya kwa uwekezaji wa raslimali zaidi katika vita dhidi ya matumizi ya pufya,” alisema Muingereza huyo, akiongeza kuwa njia moja ya Kenya kupunguza visa hivyo ni ushirikiano wa pamoja na wadau wote wa michezo chini.

Namwamba kwa upande wake pia alipongeza Coe kwa kuona juhudi za Kenya katika vita dhidi ya uovu huo.

Waziri huyo alifichua Jumatano iliyopita kuwa serikali itaongeza Sh619 milioni katika vita dhidi ya matumizi ya pufya kwa kipindi cha miaka mitano.

Namwamba alisema kuwa Shirikisho la Riadha Kenya AK na ADAK zitatumia fedha hizo katika kuimarisha uwezo wa kupima, hamasisha, uchunguzi na utekelezaji.

“Pia, zitasaidia katika kusajiliwa kwa makocha na kambi za mazoezi,” alisema Namwamba, akisisitiza kuwa serikali inaheshimu na kuchukulia kwa uzito haki za wanamichezo wote kushiriki michezo bila ya kutumia dawa za kusisimua misuli.

Aliapa pia kukabiliana na uovu huo kama kosa sawa na wahalifu wa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Wakenya waliopokea marufuku 2022 kwa kuvunja sheria zinazokataza wanamichezo kutumia dawa za kusisimua misuli ni wanariadha Lilian Kasait, Diana Kipyokei, Betty Lempus, Vane Nyaboke, Eglay Nalyanya, Joyce Chepkirui, Purity Jerono, Tabitha Wambui, Ibrahim Wachira, Kenneth Renju, Philemon Kacheran, Mark Kangogo, Lawrence Cherono, Felix Kipchumba, Emmanuel Saina, Johnstone Maiyo, Michael Kunyuga, Joel Mwangi, Morris Gachaga, Matthew Kisorio, Justus Kimutai, Daniel Wanjiru, Paul Lonyangata, Edward Kiprop na bondia Michael Odhiambo.

You can share this post!

ZARAA: Mfumo ulioboreshwa kuendeleza kilimo mijini

DRC kuandaa uchaguzi mkuu mzozo ukichacha

T L