• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Denmark wabandua Jamhuri ya Czech kwenye robo-fainali za Euro kwa kichapo cha 2-1

Denmark wabandua Jamhuri ya Czech kwenye robo-fainali za Euro kwa kichapo cha 2-1

Na MASHIRIKA

SAFARI ya Jamhuri ya Czech kufuzu kwa nusu-fainali za Euro mwaka huu ilikatizwa ghafla na Denmark waliowapokeza kichapo cha 2-1 mnamo Jumamosi jijini Baku, Azerbaijan.

Tangu mchuano wao wa ufunguzi wa Euro dhidi ya Finland katika Kundi B ukamilike kwa masikitiko ya kiungo Christian Eriksen kuanguka na kuzimia uwanjani kutokana na mshtuko wa moyo, Denmark wamekuwa wakiimarika katika kila mechi.

Ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya Urusi katika mchuano wa mwisho kundini uliwakatia tiketi ya kuvaana na Wales kwenye hatua ya 16-bora licha ya Ubelgiji kuwacharaza 2-1 katika mechi ya pili ya Kundi B.

Denmark waliwakomoa Wales 4-0 na kufuzu kwa robo-fainali dhidi ya Jamhuri ya Czech. Kikosi hicho kwa sasa kinajiandaa kwa nusu-fainali dhidi ya Uingereza waliowapepeta Ukraine 4-0 kwenye robo-fainali nyingine mnamo Jumamosi.

Wakicheza dhidi ya Jamhuri ya Czech, Denmark walifungua ukurasa wa mabao kupitia Thomas Delaney katika dakika ya tano kabla ya Kasper Dolberg kushirikiana na Joakim Maehle na kufanya mambo kuwa 2-0 mwishoni mwa kipindi cha pili.

Fowadi Patrik Schick alifutia Jamhuri ya Czech machozi mwanzoni mwa kipindi cha pili. Bao hilo alilolifunga katika dakika ya 49 lilikuwa lake la tano kwenye kampeni za Euro mwaka huu huku idadi hiyo ya mabao ikiwiana na ya Cristiano Ronaldo wa Ureno.

Wawili hao wangalipo kwenye vita vya kufukuzia taji la mfungaji bora licha ya timu zao kubanduliwa.

Takriban miongo mitatu imepita tangu Denmark waduwaze mashabiki kwa kujizolea taji la Euro mnamo 1992.

Kikosi hicho kilikuwa kimesakata soka ya Euro mwaka huu kwa dakika 41 pekee kabla ya Eriksen kuzimia uwanjani katika mchuano uliorejelewa baada ya saa mbili na kukamilika kwa Finland kusajili ushindi wa 1-0 mnamo Juni 12.

Ingawa bao la Jamhuri ya Czech katika dakika ya 49 liliwapa motisha ya kuvamia zaidi wapinzani wao, Denmark walisalia imara katika ngome yao huku kipa Kasper Schmeichel na mabeki Andreas Christensen, Simon Kjaer pamoja na Jannick Versergaard wakishirikiana vilivyo.

Ushindi wa Denmark dhidi ya Jamhuri ya Czech ulikuwa wao wa kwanza kwenye Euro na ulitosha kuwapa fursa ya kulipiza kisasi ya kubanduliwa kwenye robo-fainali za kipute hicho mnamo 2004. Mabao mawili kutoka kwa Milan Baros wakati huo yalisaidia Jamhuri ya Czech kuwakomoa Denmark 3-0.

Baros alikamilisha kampeni hizo za Euro 2004 na mabao matano kapuni mwake, idadi ambayo kwa sasa inajivuniwa na Schick ambaye anatarajiwa kustaafu kwenye soka ya kimataifa mwaka huu wa 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kenya Simbas yararuliwa na Terenga Lions ya Senegal raga ya...

Mawakili walaani kuhangaishwa kwa Khaminwa