• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Dereva wa magari ya langalanga Lewis Hamilton sasa atakuwa akiitwa ‘Sir’

Dereva wa magari ya langalanga Lewis Hamilton sasa atakuwa akiitwa ‘Sir’

Na MASHIRIKA

BINGWA mara saba duniani wa mbio za magari ya Langalanga (Formula One), Lewis Hamilton ametambuliwa nchini Uingereza kwa ukubwa na upekee wa mchango wake kitaaluma na sasa ataitwa ‘Sir’.

Mwanamichezo huyo mwenye umri wa miaka 35 alitambuliwa na kutuzwa kwa mafanikio ya kuwa dereva bora wa muda wote katika F1 baada ya kufikia na kuivunja rekodi ya mataji saba ya Mjerumani Michael Schumacher (Ferrari) aliyeshinda jumla ya mashindano 91 mfululizo.

Akiendesha magari aina ya Mercedes, Hamilton ambaye ndiye dereva wa pekee mweusi wa F1, alizaliwa na kulelewa katika familia isiyojiweza miongoni mwa wahamiaji wa nchi za Caribbean. Amekuwa akitumia mfano wa makuzi yake ya ujanani na mafanikio yake kitaaluma kuhamasisha dhidi ya ubaguzi wa rangi na dhuluma katika jamii.

Nyota huyo ndiye mwanamichezo wa pekee aliyeunga orodha ya watu waliotambuliwa na kuanza kuitwa Sir katika orodha hiyo ya Disemba 31, 2020 huku wengi wakituzwa kutokana na mchango wao katika kukabiliana na janga la corona.

Ufanisi wa Hamilton umepokelewa vyema na kusherehekewa pakubwa na mashabiki wake kote duniani na zaidi nchini Uingereza na Ufaransa.

“Hamilton ni miongoni mwa wanamichezo ambao ushawishi wao unahisika zaidi ndani na nje ya ulingo wa mbio za magari,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa F1, Stefano Domenicali ambaye aliwahi kuendesha magari aina ya Ferrari katika enzi zake za kushindana.

Kinara wa kikosi cha Mercedes, Toto Wolff alikuwa mwingi wa sifa kwa Hamilton aliyenyanyua taji lake la kwanza akiwakilisha kikosi cha McLaren mnamo 2008.

“Ndiye mwanamichezo bora zaidi wa enzi yake nchini Uingereza. Tunamstahi sana kwa kuwa sasa atakuwa akiitwa Sir Lewis Hamilton,” akasema.

Hamilton ni dereva wa nne wa F1 kuwahi kutambuliwa na kufikia hadhi ya kuitwa Sir baada ya Stirling Moss, bingwa mara tatu Jackie Stewart na marehemu Jack Brabham aliyekuwa raia wa Australia.

Wanamichezo wengine waliowahi kutambuliwa na kutuzwa kiasi hicho ni bingwa wa dunia katika mbio za uendeshaji baiskeli za Tour de France Bradley Wiggins, mshindi wa mbio za mita 5,000 na mita 10,000 kwenye Olimpiki Mo Farah, bingwa mara mbili wa tenisi za Wimbledon Andy Muuray na nyota wa kriketi nchini Uingereza, Alastair Cook.

You can share this post!

Kibarua kigumu kwa wanavoliboli wa Kenya kimataifa baada ya...

Covid-19 yavuruga maandalizi ya timu ya taifa ya Zimbabwe...