• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Difenda Dani Alves kuagana na Barcelona kwa mara ya pili

Difenda Dani Alves kuagana na Barcelona kwa mara ya pili

Na MASHIRIKA

BEKI mzoefu raia wa Brazil, Dani Alves, amethibitisha kwamba ataagana na Barcelona kwa mara ya pili baada ya kurejea kambini mwa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo 2021.

Alves, 39, alijiunga upya na Barcelona mnamo Novemba 2021, miaka mitano baada ya kuondoka ugani Camp Nou na kuyoyomea Italia kuvalia jezi za Juventus.

Kijumla, nyota huyo amechezea Barcelona mara 407 na kunyanyua mataji sita ya La Liga.

Katika miaka minane ya kwanza kambini mwa Barcelona, Alves alinyanyua pia mataji ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara tatu na kuzoa mataji manne ya Copa del Rey kati ya makombe 23 anayojivunia katika taaluma yake ya usogora.

Beki huyo wa kulia alisaidia Juventus kutwaa taji la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo 2016-17 kabla ya kutua Ufaransa ambapo aliosaidia Paris Saint-Germain (PSG) kutia kapuni taji la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo 2017-18 na 2018-19.

Kabla ya kurejea Barcelona, alikuwa amechezea kikosi cha Sao Paulo nchini Brazil.

Alipangwa katika kikosi cha Brazil kilichoshinda Japan na Korea Kusini mnamo Juni 2022 na anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachotegemewa na Brazil kwenye fainali za Kombe la Dunia mnamo Novemba-Disemba 2022 nchini Qatar.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wachezaji 10 wa EPL katika orodha ya chipukizi 100...

KIKOLEZO: Cannes Festival ni hivi na hivyo!

T L