• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
Dkt Ruto asema ni kufa kupona Harambee Stars ikikwaana na Misri

Dkt Ruto asema ni kufa kupona Harambee Stars ikikwaana na Misri

Na MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais Dkt William Ruto amekiri kipute cha leo saa moja usiku kati ya Harambee Stars na Misri kitakuwa kigumu kiasi kwamba vijana wa nyumbani watahitaji maombi na imani kuibuka washindi.

Amesema kibarua kilichoko mbele ya Kenya ni kigumu kwa sababu vijana wa nyumbani wanacheza dhidi ya miamba Misri lakini “mimi kama mwenye imani kwa Maulana ninawatakia mema.”

Amewapa kidokezo kuwa ikiwa wanataka kuibuka na ushindi, “wekeni ngome thabiti ili hasa straika Mohamed Salah anayesakatia klabu ya Liverpool inayoshiriki EPL asiwe na nafasi ya kutuumiza mbele ya lango letu.”

Kipute hicho cha kubainisha mbivu na mbichi katika Kundi G kusaka tiketi ya kuwakilisha taifa katika gozi la Ubingwa wa Bara Afrika baadaye mwaka huu katika taifa la Camoroon kitachezewa ugani Kasarani.

Kenya inatazamiwa kuweka mchezoni nyani Ian Otieno, kiungo Joshua Onyango, huduma za ugavi gozi zikiwajibishwa Anthony Akumu na Cliff Nyakeya huku Michael Olunga mhandisi akiwajibikia upachikaji na kuwapa raha mashabiki.

Cha kuwapa mashabiki wa vijana wa nyumbani kiwewe ni kwamba masogora walio na tajriba kama Victor Wanyama, Johannah Omollo, Eric Omondi na Ayub Timbe hawako katika orodha ya watakaotumika kama vifaa dhidi ya Misri.

Upande wa Misri ni hatari ya Salah mwenyewe akisaka magoli pamoja na Mohamed El-Shennawy anayesakatia klabu ya El Ahly.

Kenya iko katika nafasi ya tatu katika kundi hili ikiwa na alama tatu na inahitaji ushindi dhidi ya Misri na hatimaye itandike Togo.

Kocha Jacob Ghost Mulee tayari amekiri kuwa “binafsi niko, kwa ujumla kama timu tuko na kibarua.”

Misri ni miongoni mwa timu bora zaidi barani Afrika.

You can share this post!

Kilifi Ladies FC Yaanzishwa Kuwasaidia Wasichana Wajiepushe...

Jamhuri ya Czech yaponda Estonia bila huruma katika mechi...