• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Fataki ya Olunga dhidi ya Al Ahli Saudi linawania goli bora la mechi za makundi za Klabu Bingwa Asia, kura zinaendelea

Fataki ya Olunga dhidi ya Al Ahli Saudi linawania goli bora la mechi za makundi za Klabu Bingwa Asia, kura zinaendelea

Na GEOFFREY ANENE

MASHABIKI wa Kenya na soka kwa jumla wana hadi Mei 8 kupigia mshambuliaji Michael Olunga kura ya kutafuta mshindi wa tuzo ya goli safi la mechi za makundi ya Klabu Bingwa Asia za ukanda wa Magharibi.

Fataki ya frikiki kutoka karibu mita 23 kutoka kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 chini ya ukuta wa wenyeji Al Ahli Saudi liliweka miamba wa Qatar Al Duhail kifua mbele 1-0 dakika ya 60 ugani King Abdullah mjini Jeddah mnamo Aprili 30.

Mechi hiyo ya mwisho ya vijana wa kocha Sabri Lamouchi ilitamatika 1-1 baada ya Haitham Asiri kusawazishia Al Ahli, huku pande hizo mbili zikibanduliwa kwenye dimba hilo.

Esteghlal kutoka Iran ilinyakua tiketi ya moja kwa moja kutoka kundi hilo ya kushiriki michuano ya raundi ya 16-bora.

Bao hilo la Olunga lilikuwa la tisa katika mashindano hayo. Anasalia juu ya jedwali la wafungaji wa mabao akiwa amefungua mwanya wa magoli manne dhidi ya mpinzani wake wa karibu Cheick Diabate (Esteghlal).

Olunga anawania tuzo ya goli safi dhidi ya Mhispania Santi Cazorla (Al Sadd) aliyemwaga kipa wa Al Nassr, Brad Jones pia kupitia ikabu katika mechi ya Kundi D mnamo Aprili 29. Al Nassr ilishinda 2-1 na kubandua mabingwa hao wa Qatar kutoka kipute hicho.

Wachezaji wengine wanaowania tuzo hiyo ni Mohammad Abbaszadeh (Tractor FC), Sharof Mukhiddinov (Pakhtakor), Mehdi Ghaedi (Esteghlal), Abderrazak Hamdallah (Al Nassr), Carlos Eduardo (Shabab Al Ahli Dubai) na Shahriyar Moghanlou (Persepolis). Upigaji huo wa kura, ambao unafanywa kwenye tovuti ya Shirikisho la Soka barani Asia (AFC) ulianza Mei 4. Piga kura hapa https://www.the-afc.com/competitions/afc-champions-league/latest/news/vote-for-your-best-goal-of-2021-afc-champions-league-west-group-stage

  • Tags

You can share this post!

Lapsset kufunguliwa mapema kuliko jinsi ilivyotarajiwa

Bunge la Kitaifa lapitisha Mswada wa BBI