• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 8:11 PM
Bunge la Kitaifa lapitisha Mswada wa BBI

Bunge la Kitaifa lapitisha Mswada wa BBI

Na CHARLES WASONGA

BUNGE la Kitaifa Alhamisi usiku ilipitisha Mswada wa Mageuzi ya Katiba kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI) baada ya jumla ya wabunge 224 kuunga mkono.

Nao wabunge 63, wengi wao wakiwa wa mrengo wa ‘Tangatanga’ walipiga kura ya LA huku wabunge wawili wakisusia shughuli hiyo, katika awamu ya tatu, yaani third reading. Shughuli hiyo ilitamatika saa tano na dakika 50 za usiku. Jumla ya wabunge 320 walishiriki shughuli hiyo.

Katika awamu ya pili, jumla ya wabunge 235 walipiga kura ya NDIO huku 83 wakipiga kura ya LA kwa Mswada huo wa BBI. Wawili, akiwemo mbunge wa Kuresoi Kaskazini na Naibu Spika Moses Cheboi, wakisusia shughuli hiyo.

Jumla ya wabunge 289 walikuwepo wakati wa upigaji kura ambao uliendeshwa moja kwa moja na kupitia mtandaoni.

Sasa macho yanaelekezwa katika Bunge la Seneti ambapo maseneta wanatarajiwa kuamua hatima ya Mswada huo mnamo Jumanne wiki ijayo. Hata hivyo, mgawanyiko mkubwa umeibuka miongoni mwa maseneta hao huku baadhi yao wakishikilia kuwa sharti waufanyie marekebisho mswada huo.

Spika Kenneth Lusaka anatarajiwa kutoa uamuzi Jumanne asubuhi kama maseneta hao wanaweza kufanya marekebisho yoyote kwa Mswada huo.

Kipengele cha 257 cha Katiba kinasema Mswada kama huo unafaa kuasisiwa na wananchi wenyewe.

Sasa mswada huo utawasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta endapo mahakama haitaweka vikawazo vyovyote.

Kuna kesi kadhaa zinazopinga uhalali wa Mswada wa BBI. Moja ya kesi hizo inazuia mabunge mawili kuwasilisha Mswada huo kwa Rais Kenyatta na nyingine inazuia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuandaa kura ya maamuzi kuhusu Mswada huo.

You can share this post!

Fataki ya Olunga dhidi ya Al Ahli Saudi linawania goli bora...

Mbungo kupanga upya mikakati ya kuinoa timu yake ya Bandari...