• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Gaspo Women wako ngangari kutwaa ubingwa, watuma salamu kwa wapinzani wao katika KWPL

Gaspo Women wako ngangari kutwaa ubingwa, watuma salamu kwa wapinzani wao katika KWPL

NA AREGE RUTH

MKUFUNZI wa Gaspo Women ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL) James Ombeng’, amethibitisha kuwa wana uwezo wa kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.

Gaspo walishuka hadi nafasi ya pili baada ya sare tasa dhidi ya Nakuru City Queens. Sare hiyo iliwafanya wadondoshe pointi tena katika kinyang’anyiro cha kuwania taji.

“Tuna matumaini makubwa kuhusu kushinda ligi. Hatuna presha kwa sababu tuna pointi sawa na washindani wetu wa karibu. Kwa sasa tunarudi kurekebisha makosa yetu kuendelea kujiandaa kwa mchezo wetu ujao,” alisema Ombeng’.

Vihiga Queens walipanda hadi kileleni mwa jedwali na alama 24 baada ya ushindi wa 5-0 dhidi ya Kangemi Ladies. Alama sawa na Gaspo lakini wanatofautiana na mabao mawili.

Mabingwa watetezi Thika Queens wanafuata katika nafasi ya tatu na alama 25. Nakuru na wanajeshi wa Ulinzi Starlets wanashikilia nafasi ya nne na tano wakiwa na alama 24 na 21 mtawalia.

Kwingineko, ugani Camp Toyoyo jijini Nairobi, kizaazaa kilishuhudiwa baada ya wachezaji watano kupata kadi nyekundu kwenye mechi kati ya Kayole Starlets na Wadadia Women.

Wachezaji hao wa Kayole ni Faria Ngadira, Lorna Oduori na Sabeti. Viungo Jackline Chesang na Kiungo Mercy Anyango kutoka Wadadia pia walipata adhabu hiyo.

Ugani Moi jijini Kisumu, mechi kati ya Kisumu All Starlets na Bunyore Starlets, beki wa Bunyore  Priscah Ambale alipata kadi nyekundu baada ya kunawa mpira kwenye kijisanduku.

Kayole wako mkiani kwenye jedwali bila alama, chini ya kocha Collins Tiego.

Tiego anasema mechi hiyo ilikuwa na presha kupita kiasi.

“Mechi ilikuwa na mambo mengi kutoka mwanzoni. Baadhi ya wachezaji ambao walicheza ni sajili mpya na kila mmoja alitaka kuonyesha uwezo wake. Sasa tutakosa huduma zao katika mechi tatu zijazo,” alisema Tiego.

“Wakati huu wa dirisha uhamisho nimeachilia wachezai 16 na tayari nimefanya sajili ya wachezaji tisa. Ifikapo kesho pia nitaongeza wachezaji wengine wawili,” aliongezea Tiego.

  • Tags

You can share this post!

Matiang’i apumua baada ya msamaha

Polisi wapoteza bunduki wakijipiga ‘selfie’

T L