• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Hali ya Man City si shwari tena

Hali ya Man City si shwari tena

NA MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MCHECHETO umeikumba klabu ya Manchester City baada ya kubainika kuwa huenda ikaadhibiwa vikali kwa makosa kadhaa ya ukiukaji wa masharti ya matumizi ya kifedha.

Japo kocha Pep Guardiola alielezea imani yake kuwa makosa hayo ni uzushi, alieleza kuwa iwapo atabaini waajiri wake walimdanganya, atajiondoa klabuni humo mara moja.

“Klabu hii inapohusishwa na hatia, huwa ninawauliza; ‘Niambieni kuhusu madai hayo’ . Huwa wananielezea nami ninawaamini. ‘Niliwaambia; ‘Mkinidanganya, siku inayofuatia sitakuwa nanyi tena. Nitajiondoa wala sitakuwa rafiki wenu tena’.”

Taarifa kuhusu madai hayo imeorodhesha mashtaka 100 ambayo huenda yakachangia klabu hiyo kupigwa marufuku kutoka Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Mashtaka hayo yanahusiana na ukiukaji wa kanuni kwa misimu 14 ambapo uchunguzi ulioanza Desemba 2018 umeonyesha jinsi klabu hiyo ilivyoficha rekodi za malipo ya wachezaji na kocha, pamoja na stakabadhi za matumizi yake ya kifedha kwa jumla.

Tume iliyofuatilia madai hayo inatarajiwa kupendekeza klabu hiyo iadhibiwe vikali, adhabu ambayo ni pamoja na kuondolewa kabisa kwenye ligi kuu ya EPL, kupigwa marufuku kwa muda usiojulikana, kupigwa faini ya pesa nyingi, au kupokonywa pointi ligini.

Hata hivyo, kwenye taarifa yake, klabu hiyo imesema kwamba imeshangazwa na madai hayo huku ikisisitiza kwamba ina ushahidi wa kutosha kujitetea.

Gazeti la Sunday Times limedai kwamba Manchester City haiwezi kukata rufaa dhidi ya adhabu ya EPL kwenye Mahakama ya kusuluhisho mizozo michezoni kule Uswisi ambayo ilibatilisha kufungiwa kwa klabu hiyo kushiriki katika michuano ya Klabu Bingwa barani Ulaya mnamo 2020.

Utafiti umefanywa ambapo imegunduliwa kwamba Man City iko katika nafasi ya sita kwa utajiri ulimwenguni, na ya tatu nyuma ya Manchester United na Liverpool kwenye ligi kuu ya EPL.

Wamiliki wakuu wa Manchester City ni City Football Group, chini ya bwanyenye Sheikh Mansour bin Zayed Al Nahyan, ambayo ni kati ya familia tajiri zaidi eneo la Mashariki ya Kati (UAE).

Adhabu inayotarajiwa kuchukuliwa Manchester City imekuja siku chache tu baada ya bwanyenye Mwaamerika Todd Boehly kununua Chelsea kwa zaidi ya Sh600 bilioni kutoka kwa tajiri wa mafuta Roman Abramovich wa Russia.

Kadhalika umetokea wakati ambapo wamiliki wa Manchester United na Liverpool wanafikiria kuuza klabu hizo. Manchester City walitwaa ubingwa wa EPL misimu miwili iliyopita, na kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili jedwalini msimu huu wa 2022/2023, nyuma ya Arsenal kwa tofauti ya pointi tano.

  • Tags

You can share this post!

Nguo kuchanika K’Ogalo wakionana na Tusker FC

Gavana Sakaja aahidi kuwaajiri maafisa wa kitengo cha...

T L