• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 9:50 AM
Hatuhitaji Haaland na hatuna mpango wa kuuza Lewandowski – Bayern Munich

Hatuhitaji Haaland na hatuna mpango wa kuuza Lewandowski – Bayern Munich

Na MASHIRIKA

RAIS wa Bayern Munich, Herbert Hainer, 67, amethibitisha kwamba kikosi hicho kimejiondoa kwenye mbio za kumsajili fowadi chipukizi raia wa Norway, Erling Braut Haaland kutoka Borussia Dortmund.

Aidha, amekiri kwamba Bayern hawana nia yoyote ya kumwachilia mshambuliaji wao tegemeo Robert Lewandowski kuondoka uwanjani Allianz Arena licha ya kuhemewa pakubwa na Chelsea.

Kujiondoa kwa Bayern katika vita vya kufukuzia huduma za Haaland ni habari njema kwa Chelsea ambao kwa pamoja na Manchester City, wamekuwa wakikeshea maarifa ya nyota huyo wa zamani wa RB Salzburg ya Austria.

Hainer amesisitiza kuwa Lewandowski ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Poland, sasa atasalia kambini mwa Bayern hadi mkataba wake utakapotamatika rasmi mnamo Juni 2023.

“Lewandowski atachezea Bayern hadi Juni 2023. Angali na mkataba nasi na ataendelea kuwa hapa Allianz Arena. Hatuna haja ya kutafuta mshambuliaji mpya wa kumrithi,” akaongeza Hainer.

Lewandowski ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Dortmund anajiandaa sasa kuanza msimu wake wa nane kambini mwa Bayern aliowafungia jumla ya mabao 41 mnamo 2020-21.

Kocha Thomas Tuchel wa Chelsea amefichua mpango wa kumshawishi Romelu Lukaku wa Inter Milan kujiunga nao iwapo juhudi zao za kumsajili Haaland zitazaa nunge. Lukaku aliwahi kuchezea Chelsea hadi 2014 kabla ya kuhamia Everton kisha Manchester United.

Chelsea waliokuwa radhi kuweka mezani kima cha Sh7.8 bilioni kwa ajili ya maarifa ya Lewandowski, wameratibiwa kuanza kampeni zao za msimu wa 2021-22 dhidi ya Crystal Palace mnamo Agosti 14.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Basari za matajiri

MATHEKA: Miungano mipya ya kisiasa isiwe ya kupiganisha raia