• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 AM
Hoki: Butali Warriors yapiga Sailors kurejea kileleni, Mashujaa yatesa Mombasa Sports Club

Hoki: Butali Warriors yapiga Sailors kurejea kileleni, Mashujaa yatesa Mombasa Sports Club

NA JOHN KIMWERE

WAFALME wa magongo nchini, Butali Warriors walirejea kileleni mwa Ligi Kuu msimu huu baada ya kuzoa alama tatu muhimu kwenye mechi za wikendi.

Butali Warriors ya kocha Geoffrey Wakachangwa ilipiku wapinzani wao Kenya Police ilipovuna ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sailors ugani City Park, Nairobi.

Butali ilipata ushindi huo kupitia juhudi za Festus Onyango na Francis Kariuki huku Johnstone Indiazi akifungia Sailors goli la kufuta machozi.

Nayo Mombasa Sports Club (MSC) ilirejea makwao mikono mitupu baada ya kupoteza mechi zake mbili. Wanaume hao waligaragazwa kwa mabao 7-0 na Western Jaguars kabla ya kudungwa mabao 3-2 na Mashujaa ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha USIU.

Nahodha wa Mashujaa ya Chuo Kikuu cha Kimataifa cha USIU, Jamleck Macharia akipiga mpira walipokabili Mombasa Sports Club (MSC) kwenye magongo ya wanaume ya Ligi Kuu ugani City Park, Nairobi mnamo Jumapili. USIU ilishinda kwa mabao 3-2. PICHA | JOHN KIMWERE

Nayo Wazalendo iliangukia pua iliponyukwa mabao 4-1 na Gladiators ya Chuo Kikuu cha Strathmore.

”Tunafuraha tumerejea kileleni mwa jedwali tunakolenga kukaza buti kuhakikisha tunahifadhi taji hilo kwa mara ya tatu mfululizo,” kocha wa Butali, Geoffrey Wakachangwa alisema na kutoa wito kwa vijana wake kuwa makini zaidi kwenye mechi zijazo.

Huku ikiwa imesalia mechi moja kukamilisha mkumbo wa kwanza, Butali Warriors inaongoza kwa kusajili alama 20, moja mbele ya mahasimu wao Kenya Police baada ya kushiriki patashika nane kila moja.

Wanazuo wa Strathmore wamefunga tatu bora kwa alama 13 sawa na Wazalendo kutokana na mechi nane na saba mtawalia. Sailors ingali katika nafasi ya tano kwa kusajili pointi 11, sawa na USIU-A baada ya kucheza mechi saba na nane mtawalia.

 

  • Tags

You can share this post!

UJASIRIAMALI: Agundua siri kupunguza gharama ya juu ya...

Kinyang’anyiro 2022: Kaunti ya Lamu

T L