• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 7:50 AM
Kinyang’anyiro 2022: Kaunti ya Lamu

Kinyang’anyiro 2022: Kaunti ya Lamu

NA KALUME KAZUNGU

LAMU ni kaunti nambari 005 iliyo kaskazini mwa Pwani ya Kenya.

UKUBWA: Kilomita 6,273 mraba.

IDADI YA WATU: 142,920 kulingana na ripoti ya sensa ya mwaka 2019.

WAPIGA KURA: 79,157.

MAENEO BUNGE: Lamu Magharibi na Lamu Mashariki.

Kaunti ya Lamu iko na Wadi 10 zifuatazo; Mkomani, Shela, Bahari, Hongwe, Mkunumbi, Witu, Hindi, Basuba, Kiunga na Faza.

Gavana wa sasa ni Fahim Yasin Twaha (Jubilee) anayetafuta fursa nyingine Agosti 9.

Lamu ni mwenyeji wa Bandari ya pili nchini chini ya mpango wa uchukuzi wa serikali kutoka Kenya, ikiunganisha Ethiopia na Sudan Kusini (LAPSSET).

Inasifika kwa turathi nyingi za kitaifa na fuo safi za Bahari Hindi. Uchumi wa Lamu hutegemea uvuvi, utalii, biashara, kilimo na ufugaji.

Vijana wakijumuika kwenye kampeni ya kusafisha fuo za Bahari Hindi mjini Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

CHANGAMOTO

Utovu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab kutoka nchi jirani ya Somalia.

Miundomsingi duni, hasa ya uchukuzi.

Ukosefu wa ardhi na hatimiliki.

Dawa za kulevya miongoni mwa vijana.

UGAVANA

1. Fahim Yasin Twaha (Jubilee/Azimio One Kenya)

Ni gavana wa pili aliyeingia 2017.

Alizaliwa Mei 14, 1968, (umri wa miaka 54).

Ana digrii ya masuala ya uchumi na shahada ya uzamifu kuhusiana na usimamizi wa biashara (MBA) kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Amedumu siasani kwa karibu miaka 25.

Alianza siasa zake 1997, akiwania na kushinda kiti cha eneobunge la Lamu Magharibi kupitia KANU hadi 2013 aliposhindwa ugavana na mtangulizi wake Issa Timamy.

MANIFESTO: Kuinua elimu ili watoto wengi wajiunge na shule za sekondari, vyuo vikuu na taasis anuwai kupitia ufadhili wa karo kutoka kwa serikali ya kaunti.

Maskwota kupewa ardhi na hatimiliki, kuinua kilimo, utalii, biashara, afya na ufugaji, kupanua uvuvi kupitia ufadhili na utoaji wa vifaa vya kisasa kwa wavuvi, kuinua miundomsingi ya maji.

2. Issa Abdallah Timamy (ANC/KENYA KWANZA)

Alizaliwa Septemba 1959, (miaka 63).

Ni gavana wa kwanza wa Lamu kati ya 2013 hadi 2017.

Alijitosa siasani 2013 na kushinda kiti cha ugavana kupitia UDF.

Gavana wa zamani wa Lamu, Issa Timamy (kulia) wa chama cha ANC na Kenya Kwanza akiwa na mgombea mwenza Raphael Munywa. Ni miongoni mwa wanaotafuta ugavana wa Lamu, Agosti 9, 2022. PICHA | KALUME KAZUNGU

Taaluma yake ni Uanasheria, akiwa amesomea Chuo Kikuu cha Nairobi.

Kabla ya siasa, aliwahi kuhudumu kama mwenyekiti wa Halmashauri ya Turathi za Kitaifa nchini (NMK).

MANIFESTO:

Kupigania haki za ardhi, elimu kwa wote, afya bora, ajira kwa vijana, kuboresha utalii, kilimo, biashara na ufugaji.

3. Eric Mugo Kinyua (Narc Kenya/Azimio la Umoja One Kenya)

Alizaliwa Disemba 29,1983, (miaka 39).

Ana Digrii ya Sayansi na Uzamifu kuhusu michezo kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta.

Eric Mugo (akipokea cheti) wa chama cha Narc Kenya kinachoongozwa na Martha Karua. Ni miongoni mwa wagombea wanne wa kiti cha ugavana wa Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Alijiunga na siasa 2012 akiwa chuoni na 2013 akawa Naibu Gavana wa Dkt Timamy.

MANIFESTO: Kuinua maisha ya vijana wenzake, kuwatetea wapate ajira, kupigana na janga la mihadarati, kuinua elimu, kujenga viwanda na kupiga jeki uwekezaji Lamu.

4. Umra Omar Bwana (Safina)

Alizaliwa Mombasa 1983 na kulelewa kijiji cha Tchundwa, Lamu Mashariki.

Ana digrii ya Masuala saikolojia na viungo kutoka Oberlin College jijini Ohio, Marekani na shahada ya uzamifu ya masuala ya haki na uhusiano wa kimataifa.

Umra Omar wa chama cha Safina. Ndiye mgombea wa kipekee wa kike kwenye kinyang’anyiro hicho cha ugavana Agosti 9, 2022. PICHA | KALUME KAZUNGU

Alizindua shirika lake la Safari Doctors mnamo 2014 ambalo limekuwa likitoa huduma za afya kwa wanajamii, hasa Waboni kwenye maeneo yenye changamoto za kiusalama Lamu.

MANIFESTO: Kuinua maisha ya akina mama, ajira kwa vijana, walemavu kupigwa jeki, uwekezaji kuboreshwa, kilimo, ufugaji na utalii kuimarishwa.

Bi Omar ndiye mwanamke pekee kwenye kinyang’anyiro hicho.

MAENEOBUNGE

Lamu iko na maeneobunge mawili pekee ambayo ni Lamu Magharibi na Lamu Mashariki.

Wafuatao ni wagombea kiti cha ubunge Kaunti ya Lamu, vyama vyao na maeneo wanakosimama;

LAMU MAGHARIBI

Jumla ya wagombea kumi (10) wanawania kiti hicho kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 kama ifuatavyo;

1. Stanley Muthama Muiruri (ndiye mbunge wa sasa)-Jubilee Party/Azimio la Umoja One Kenya

2. Rishad Hamid Amana-UDA/Kenya Kwanza

3. Abdu Kassim Ahmed-ANC/Kenya Kwanza

4. Hassan Albeity-PAA/Kenya Kwanza

5. Maryimmaculate Nyaga-Narc Kenya/Azimio la Umoja One Kenya

6. Josephat Musembi Matei-Usawa Kwa Wote Party

7. Zacchaeus Mboche Wanyoike-The Service Party (TSP)

8. Abdirashid Mwaura-PNU/Azimio la Umoja One Kenya

9. Khamis Kaviha- National Alliance Party of Kenya (NAPK)

10. Jannat Mohamed-United Green Movement Party (UGM)

LAMU MASHARIKI

Jumla ya wagombea wanne (4) pekee ndio wanawania kiti hicho Agosti 9, 2022 kama ifuatavyo;

1. Sharif Athman Ali (ndiye mbunge wa sasa)-UDA/Kenya Kwanza)

2. Shekuwe Kahale Kombo-KANU/Azimio la Umoja One Kenya

3. Mohamed Madhubuti-Wiper/Azimio la Umoja One Kenya

4. Ruweida Mohamed Obo-Jubilee Party/Azimio la Umoja One Kenya

MBUNGE MWAKILISHI WA KIKE

Wafuatao ndio wawaniaji wa kiti cha Mbunge Mwakilishi wa Wanawake, Kaunti ya Lamu kwenye Uchaguzi Mkuu ujao wa Agosti 9, 2022.

1. NANA MOTE

-Anawania kiti hicho kupitia chama cha Jubilee kilichoko kwenye mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya.

-Alizaliwa kijiji cha Tchundwa, Lamu Mashariki mwaka 1977.

-Alisomea Ualimu lakini baadaye akaacha kazi hiyo na kujiunga na Mamblaka ya Bandari nchini (KPA) ambako amekuwa akihudumu kama mfanyakazi wa maakuli Bandarini Mombasa.

-Aliacha kazi hiyo mwaka huu na kujitosa siasani, akitafuta uungwaji mkono wa kiti cha Mbunge Mwakilishi wa wanawake wa Lamu.

2. AMINA KALE

-Ni wa chama cha ANC kilichoko ndani ya mrengo wa Kenya Kwanza.

-Alizaliwa mtaa wa Langoni, kisiwani Lamu 1966.

-Alisomea Ualimu.

-Amekuwa akihudumu kama diwani mteule kupitia chama cha UDF na kisha ANC katika bunge la kaunti ya Lamu tangu 2013 hadi sasa.

3. ESHA NIZAR

-Ni wa chama cha ODM kilichoko mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya.

-Alizaliwa kisiwa cha Faza, Lamu Mashariki 1971.

-Alisomea na kuhitimu kozi ya masuala ya lishe.

-Kwa sasa amekuwa akifanya kazi kama mjasiriamali/mwanabiashara nchini na nje ya nchi, hasa Mashariki ya kati.

4. LOYCE DAMA LUWALI

-Ni wa chama cha Narc Kenya kilichoko mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya.

-Alizaliwa kijiji cha Vipingoni, tarafa ya Witu, Lamu Magharibi 1982.

-Ni mwanasaikolojia na mhisani wa kijamii.

5. MARYAM ABUBAKAR

-Anawania kiti hicho kupitia tikiti ya PAA.

-Alizaliwa 1980 mtaani Mkomani, kisiwa cha Lamu.

-Amesomea uhasibu na pia masuala ya usimamizi na mipango.

-Amejitosa kwenye shughuli za kibiashara, akimiliki na kuendesha kampuni yake ya Myra Botanics inayohusika na masuala ya fasheni, mapambo na ulimbwende.

6. MONICA MUTHONI MARUBU

-Alizaliwa 1989.

-Alisomea masuala ya Uhusiano wa Kimataifa (International Relations)

-Aliwahi kuhudumu kama diwani mteule wa chama cha TNA katika Bunge la Kaunti ya Lamu kati ya 2013 na 2017.

-Amekuwa akifanya kazi kama afisa wa uhusiano mwema wa kijamii katika mradi wa Bandari ya Lamu (LAPSSET).

USENETA

Kiti cha useneta katika uchaguzi mkuu ujao wa Agosti 9, 2022 kimewavutia jumla ya wagombea tisa (9) ambao tayari wameidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC).

Wafuatao ni wagombea hao tisa, vyama vyao na maelezo mafupi kuwahusu;

1. Anuar Loitiptip

-Ndiye seneta wa sasa wa Lamu aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza 2017 kupitia chama cha Jubilee.

-Anatetea kiti hicho Agosti 9, 2022 akiwa mgombea huru.

-Alizaliwa Mpeketoni, Mei 16, 1986.

-Alisoma na kuhitimu kozi ya Uhusiano Mwema wa Kimataifa na Masuala ya Amani na Uwiano (International Relations and Diplomacy katika chuo Kikuu cha Kampala International University nchini Uganda.

-Mbali na siasa, yeye pia ni mfanyabiashara.

2. Francis Kariuki Mugo

-Alizaliwa Mpeketoni, Lamu Magharibi 1990.

-Alisomea shule ya msingi ya Uzida na sekondari ya Mpeketoni.

-Alisomea na kuhitimu shahada ya masuala ya Biashara na Uhasibu katika chuo anuwai cha Technical University of Mombasa (TUM).

-Kwa sasa anasomea shahada ya Sheria chuoni University of London.

-Amekuwa akifanya kazi katika ofisi ya sheria inayomilikiwa na kampuni ya Mwaure and Mwaure Waihiga Company Advocates kabla ya kujitosa siasani.

3. Ahmed Bunu Haji

-Alizaliwa Mpeketoni, Lamu Magharibi, Mei 5,1983.

-Alisomea shule za msingi za Lake Kenyatta, Mokowe Arid Zone na kisha kumalizia shule ya Msingi ya Lamu mjini.

-Baadaye alijiunga na Shule ya Sekondari ya Shimo la Tewa mjini Mombasa.

-Alisomea na kuhitimu taaluma ya Udaktari.

-Yuko na digrii mbili za masuala ya afya.

-Pia ni mwanafunzi wa PhD katika masuala ya afya ya umma (Public Health Epidemiology) kwenye chuo kikuu cha Walden University kilichoko Marekani.

Alijitosa siasani mwaka huu na anawania useneta kupitia chama cha ODM kilichoko ndani ya Mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya.

4. Yusuf Mahmoud Aboubakar (Wakili)

-Alizaliwa kijiji cha Siyu, Lamu Mashariki 1969.

-Alisomea shule ya msingi ya Barani, Kilifi kabla ya kuhamia Serani, Mombasa alikokamilisha masomo ya msingi.

-Alijiunga na sekondari ya Shimo la Tewa, Mombasa kabla ya kusomea kozi ya Sheria chuo kikuu cha Nairobi.

-Amkuwa akifanya kazi ya Uwakili/Uanasheria kabla ya kujitosa siasani mwaka huu, akiwania kiti cha useneta kupitia chama cha ANC kilichoko ndani ya mrengo wa Kenya Kwanza.

5. Khamis Nassor Mbaruk (Bwangao)

-Alizaliwa katika kijiji cha Junju, Kilifi, 1973 na kulelewa/kukua Mpeketoni na Kibaoni, Lamu Magharibi.

-Alisomea shule ya msingi ya Tom Mboya kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Bamburi.

-Baadaye alisomea shahada ya Biashara chuo kikuu cha Nairobi.

-Ni mjasiriamali na mwanabiashara mashuhuri, akifanya kazi na shirika la mawasiliano la Airtel.

-Alijitosa siasani mwaka huu, akiwania kiti cha useneta kupitia tiketi ya chama cha KANU kilichoko mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya.

6. Joseph Githuku Kamau

-Ni mwanabiashara tajika mjini Mpeketoni, akimiliki kituo cha mafuta na maduka.

-Alisomea kozi ya biashara chuo cha Mombasa Technical University (TUM).

-Alianza siasa zake 2000.

-Amewahi kuhudumu kama diwani mteule wa bunge la kaunti ya Lamu kupitia tiketi ya chama cha Farmers Party, kati ya 2013 na 2017.

-Anawania useneta wa Lamu kupitia chama cha Jubilee.

7. Ahmed Suleiman Ali

Alizaliwa 1988, kisiwani Lamu.

-Alisomea shule ya msingi ya Tchundwa, Lamu Mashariki kabla ya kujiunga na shule ya upili ya wavulana ya Lamu.

-Baadaye alipata ufadhili wa kimasomo nchini Sudan kupitia mpango wa Kenya Education Trust Fund ambako alisomea masuala ya uchumi-enonomics.

-Amekuwa akifundisha wanafunzi kwenye chuo cha Sudan kabla ya kurudi Kenya ambako alifunza shule ya wasichana ya sekondari ya Lamu.

-Amewahi kufanya kazi kwa benki za First Community na Gulf Bank.

-Baadaye aliteukliwa msimamizi na mshirikishi wa hospitali za King Fahd, Faza na Mokowe, ambapo ni wakati huo aliongeza masomo ya shahada ya uzamifu ya masuala ya fedha (Finance) katika chuo kikuu cha Kenyatta.

-Mwaka 2020 alipata ufadhili wa kimasomo Uingereza (UK) alikosomea Masters in Development Economics.

-Pia amekuwa mshauri wa kiuchumi na kifedha nchini Uingereza kabla ya kurudi Kenya na kujitosa siasani mwaka huu, akiwania kiti hicho kupitia tiketi ya chama cha UPIA Party.

8. Abudi Omar Mohamed

-Anawania kiti cha useneta wa Lamu Agosti 9,2022 kupitia chama cha Wiper Democratic Movement kilichoko mrengo wa Azimio la Umoja One Kenya.

9. Abdiwely Mohamed Dhahir

-Alizaliwa Mpeketoni, Lamu Magharibi, 1993.

-Alisomea shule ya msingi ya Hindi na kujiunga na shule ya upili ya wavulana ya Mpeketoni.

-Alijiunga na Technical University of Mombasa ambako alisomea Digrii ya Bachelor of Science in Development Studies and Counselling.

-Amekuwa akijihusisha na masuala ya Biashara (maduka ya jumla) na ukulima eneo la Hindi, Lamu Magharibi.

-Amewahi kugombea kiti cha udiwani eneo hilo lakini akakosa.

Kwa sasa anawania kiti cha useneta katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 kupitia chama cha National Agenda Party of Kenya (NAPK).

  • Tags

You can share this post!

Hoki: Butali Warriors yapiga Sailors kurejea kileleni,...

Wajackoyah kuvumisha biashara ya bangi, nyoka

T L