• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
HOKI: Lakers yaendelea kujiimarisha iwe tishio kwa wapinzani katika Ligi Kuu

HOKI: Lakers yaendelea kujiimarisha iwe tishio kwa wapinzani katika Ligi Kuu

NA JOHN KIMWERE

KLABU ya wanawake ya Lakers ni kati ya vikosi saba vinavyoshiriki kipute cha magongo ya Ligi Kuu msimu huu.

Ingawa ndio mara ya tatu kushiriki kipute hicho inajivunia kutoa wachezaji watano ambao wamo nchini Uingereza kushiriki Michezo ya Jumuiya ya Madola.

Watano hao ambao wamo katika timu ya taifa maarufu Blades ni Alice Owiti (nahodha), Vivian Onyango, Maureen Owiti, Millicent Adhiambo na Aurelia Opondo.

”Tuna imani kwamba endapo tunaweza kupata mfadhili tuna uwezo tosha kutikisa wapinzani wengine kwenye kampeni za kipute cha msimu huu,” kocha wake, Austin Tuju akasema na kutoa wito kwa wahisani kujitokeza ili kuwapiga jeki kwenye jitihada za makuzi ya talanta za wachezaji wanaokuja kwa kasi kwenye mchezo wa magongo.

Anashikilia kuwa mvumilivu hula mbivu akiwatia nari wachezaji wake kuwa wanaelekea kuibuka malkia wa mchezo huo nchini.

Anawaambia wawe wavumilivu, watie bidii na kujituma bila kulegeza kamba hatimaye watavuna mazuri.

Kocha huyu anakariri kuwa wanajipatia miaka miwli pekee kisha ndio watakuwa wapinzani wakuu huku wakilenga kubeba ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili au tatu ndani ya miaka mitano ijayo.

La mno anasema wanatamani sana kubeba ubingwa huo ili kujikatia tikiti ya kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Afrika (CCCA).

Kwa sasa Lakers chini ya nahodha Alice Owiti inashikilia nafasi nne kwa kuzoa alama nne, moja mbele ya Amira Sailors baada ya kushuka dimbani mara tatu na nne mtawalia.

”Bila shaka tunajaribu licha ya kuwa viongozi wa ngarambe ya msimu huu wametupiku kwa alama nane,” naibu kocha, Alvin Onyangi akasema na kuongeza kuwa wamepania kujituma mithili ya mchwa kwenye mechi zijazo.

Katika msimamo huo, Scorpions ya Strathmore University inaongoza kwa alama 12 baada ya kushiriki mechi nne. Nayo USIU-A inashikilia nafasi ya pili kwa kusajili pointi saba sawa na mabingwa watetezi Blazers awali ikijulikana na Telkom Orange kutokana na mechi tatu na nne mtawalia.

Anashikilia kuwa kwenye kampeni za muhula ni timu mbili pekee zinazokaa vizuri kuwazuia kutobeba ubingwa huo ambazo ni Strathmore na USIU-A.

Lakers iliasisiwa mwaka 2017 na kocha wake, Austin Tuju akishirikiana nao John Paul Otieno na Seth Waringa. Klabu hii ambayo hufanyia mazoezi kwenye uwanja wa Shule ya Upili ya Kutwa ya Kisumu inajumuisha wachezaji kutoka maeneo tofauti ikiwamo Kisumu, Kakamega, Bungoma, Kitale, Homabay, Bondo, Maseno, Kisii, Eldoret na Kapenguria. Asilimia sabini ya wachezaji wake ni wanafunzi wa vyuo vikuu mbali mbali nchini. Meneja wake, John Paul Otieno anasema ”Licha ya pandashuka tunazopitia kifedha tunaamini tuna wachezaji wazuri wanaolenga makuu miaka ijayo.”

Orodha ya wachezaji wengine ambao wameunda timu hii inashirikisha: Maureen Achieng, Debra Otieno, Anne Wasabwa, Ashley Akinyi (naibu nahodha), Nancy Mora, Eusyla Cherotich, Francisca Koros, Stacy Chentry, Laura Ajoko, Purity Aseyo, Effie Adhiambo, Joyce Omito, Adeline Wafula, Elizabeth Awuor, Stephanie Jura, Emma Yeko, Prudence Mughala, Vivian Ogweno na Mariam Satia kati ya wengine.

 

  • Tags

You can share this post!

Maandalizi ya kura yashika kasi katika IEBC

Mary Nzula Munyao: Mwigizaji chipukizi anayelenga kumiliki...

T L